KAMPUNI ZOTE ZA MADINI NA GESI ZINATAKIWA KUFUNGASHA VIRAGO
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani amezitaka kampuni zote za madini na gesi nchini kulipa kodi stahiki na kwamba ambazo hazijaanza kupata faida mpaka sasa zifungashe virago.
Dk Kalemali alibainisha hayo juzi wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya gesi na mafuta nchini, ambao ulikuwa ukizungumzia ushirikiano wa Serikali na viwanda katika sekta ya mafuta na gesi.
Kauli hiyo inakuja wakati Serikali ikiwa katika mchakato endelevu wa kubaini upungufu uliopo katika Sekta ya madini, mpaka sasa tayari kamati nne zimefanya uchunguzi na kuwasilisha mapendekezo ambayo yanaonyesha uwapo wa udanganyifu katika uwekezaji huo.
Alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Fedha, watafanya ukaguzi katika kampuni mbalimbali ili kujiridhisha kama kweli hazipati faida.
Dk Kalemani alisema suala la kujua faida anayoipata mwekezaji ni mpaka kukaa naye na kupiga hesabu, suala ambalo TRA inatakiwa kufanya ili Watanzania waweze kunufaika na rasilimali zao.
“Kodi inayokwepwa zaidi katika sekta hizi ni baada ya kupata faida (Cooperate tax), hii inahitaji hesabu hivyo TRA na mamlaka nyingine zinazohusika zitafanya hivyo,” alisema Dk Kalemani.
Hata hivyo, wajumbe waliohudhuria mkutano huo walitoa mapendekezo namna Serikali na wazawa wanavyoweza kunufaika, kutokana na miradi inayofanyika.
Mwenyekiti wa Kampuni PanAfrican Energy Tanzania, Patrick Rutabanzibwa alisema Serikali inapaswa kuendeleza utaratibu wa kuwasomesha watu wake ili kupata ujuzi zaidi, namna shughuli hizo zinavyofanyika duniani.
“Nikiwa kijana mdogo nilikuwa nafanya kazi Wizara ya Nishati na Madini, nilipelekwa Uingereza kusoma ili miradi kama hii ikianza Serikali iwe na wataalamu wa ndani lakini kwa bahati mbaya ilichelewa mpaka nimestaafu ndiyo inakuja hii ya ujenzi wa bomba la mafuta,” alisema Rutabanzibwa.
Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya Alliend Petroleum Service limited Tanzania, Moses Asanga alisema Tanzania na nchi nyingine zenye kiu ya kuona manufaa ya mafuta na gesi, zinatakiwa kuandaa kanzi data ya kampuni za ndani ambazo mwekezaji anapaswa kuzitumia wakati wa utekelezaji mradi
No comments