Halima Mdee Apigania Haki za Watoto wa Kike
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee amesema jamii ina wajibu wa kupigania haki za watoto wa kike dhidi ya mifumo isiyokubali mabadiliko kwa kuhakikisha wanapata fursa ya kupata elimu na kushika nafasi za uongozi.
Mdee ambaye ni Mbunge wa Kawe, amepinga jitihada za kuwakwamisha wasichana wanaopata mimba wakiwa masomoni kutoendelea na masomo.
Amesema kikwazo hicho ni mojawapo ya vinavyopaswa kupewa jukwaa na wadau kutoa ufumbuzi badala ya kuwahukumu na kuwanyima nafasi ya pili.
Mdee amesema hayo katika kituo cha watoto yatima cha Samaritan Village eneo la Moshono jijini hapa alipokabidhi msaada ikiwa ni hatua ya kuunga mkono taasisi zilizojitolea kulinda haki za watoto waliokosa fursa baada ya wazazi wao kufariki dunia.
Mdee aliye jijini hapa kuongoza maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Chadema amesema kumekuwa na ukatili ndani ya jamii ambao wakati mwingine umesababisha baadhi ya wa watoto kujikuta kwenye vituo hivyo.
Amesema katika maadhimisho hayo wameamua kujishughulisha na mambo ya kijamii kwa sababu ndipo misingi ya chama chao ilipo na kimeweza kupiga hatua kisiasa kutokana na kutetea masilahi ya wanyonge na haki kwa jumla.
Mdee amesema hatatishwa wala kukata tamaa kuzungumzia mambo anayoona yanapaswa kukemewa kwa sababu ya kuogopa kukamatwa kwa kuwa yeye ni kiongozi na atatimiza wajibu wake wa kuwasemea wasioweza kusimama hadharani.
Mratibu wa kituo cha Samaritan Village, Josephat Mmanyi amesema wanalea watoto 50 wenye umri wa kuanzia mwaka mmoja hadi miaka 21 ambao wapo katika ngazi mbalimbali za masomo.
No comments