FAMILIA YA LISSU YANENA KUHUSU DEREVA
Shangazi yake Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, Ninaa Sawa(kushoto) akiwa na mama mdogo wa Lissu, Bula Muro nyumbani kwa wazazi wa Mbunge huyo Mahambe, Ikungi Singida. Picha zote na Herieth Makwetta.
Tangu kutokea kwa tukio hilo mchana wa Septemba 7 huko Dodoma, dereva wa mbunge huyo, Simon Mohamed Bakari amekuwa akitajwa kama mtu muhimu anayeweza kusimulia tukio hilo na hata kusaidia kuwabaini wahalifu.
By Herieth Makwetta, Mwananchi hmakweta@mwananchi.co.tz
Siku 10 baada ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi, familia yake imezungumzia tukio hilo na namna inavyomfahamu dereva wake kwa zaidi ya miaka 20.
Tangu kutokea kwa tukio hilo mchana wa Septemba 7 huko Dodoma, dereva wa mbunge huyo, Simon Mohamed Bakari amekuwa akitajwa kama mtu muhimu anayeweza kusimulia tukio hilo na hata kusaidia kuwabaini wahalifu.
Hata polisi imekuwa ikimtaka ili imhoji ikisema ni shahidi muhimu katika tukio hilo. Hata hivyo, kijana huyo yupo Nairobi akimuuguza bosi huku mjadala juu yake ukiendelea nchini.
Katika mahojiano na Mwananchi, familia ya mbunge huyo imeonyesha kuwa na imani kubwa na dereva hiyo ikibainisha inavyomfahamu kwa miongo miwili.
Akizungumza katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwa baba wa mbunge huyo, Lissu Mughwai katika Kijiji cha Mahambe, Kata ya Unyahati wilayani Ikungi, Singida, Muro Lissu ambaye ni kaka yake alisema hawana wasiwasi na dereva huyo kwa kuwa ni kijana aliyelelewa na mwanasheria huyo mkuu wa Chadema tangu akiwa na umri wa miaka 15.
“Yule kijana alienda kwa Lissu akiwa mdogo kama kijana wa kazi za nyumbani. Alimchukua katika Kijiji cha Sefuka kilichopo Magharibi mwa Singida. Tangu wakati huo alimfunza kazi zote akiwa pale nyumbani kwake. Amemlea, amekulia kwake,” alisema Muro.
Alisema dereva huyo alifundishwa mambo mengi akiwa mmoja wa wana familia ikiwamo kupelekwa kujifunza udereva.
Muro alisema Lissu alipoanza harakati za kuwania ubunge mwaka 2007 alikuwa na kijana huyo.
“Amekuwa dereva wake tangu alipoanza kuhangaikia jimbo mpaka amechukua ubunge mwaka 2010 akawania tena 2015. Wana miaka mingi na yule kijana zaidi ya miaka 20 amemlea,” alisema Muro.
Alisema licha ya Lissu kutozungumza chochote kuhusu vitisho alivyokuwa akipewa na kufuatiliwa na watu wasiojulikana, dereva wake alikuwa akiitaarifu familia kuhusu matukio hayo kila yalipotokea, hivyo walijua kinachoendelea kupitia kwake.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Ikungi, Jihala Ibrahim aliyekuwapo pamoja na wanafamilia katika mahojiano hayo alisema licha ya kuchanganyikiwa, dereva huyoalielezea tukio zima lilivyokuwa baada ya wao kuwasili hospitalini Dodoma wakitokea Ikungi.
“Nilikutana na dereva wake Dodoma baada ya tukio, kwa kweli yule kijana alikuwa amechanganyikiwa na mpaka anaondoka siku ya pili kwenda Nairobi alikuwa ameathirika kisaikolojia,” alisema.
Ibrahim anaamini kuwa kama asingekuwa dereva huyo, Lissu asingepona kirahisi, “Dereva wake anasema tangu wanatoka bungeni, magari mawili yalikuwa yakiwafuatilia na kila alipojaribu kuegesha gari pembeni na wao walifanya hivyo hivyo aliamua kwenda moja kwa moja nyumbani na walipofika getini gari moja lilibaki nje na lingine liliingia ndani.”
Ibrahim alisema dereva huyo aliwaeleza kuwa kabla ya watu hao kutekeleza azma yao, Lissu alikuwa tayari kushuka lakini alimzuia licha ya kutaka kushuka kwa nguvu.
“Dereva alisema baada ya kimya kifupi, gari hilo liligeuza tayari kwa kuondoka hapo alishuka mmoja wa watu hao akiwa ameficha uso wake kwa kofia na miwani myeusi, alitoa silaha na kuanza kushambulia gari la Lissu. Dereva alimwinamisha Lissu kwa nguvu kupitia nafasi iliyopo kati ya kiti chake na yeye na alifungua mlango na kujificha chini ya uvungu wa gari nyingine iliyokuwa pembeni,” alisimulia Ibrahim.
Alisema kutokana na hali ambayo alikuwa nayo kijana huyo, walilazimika kumwondoa hospitalini hapo na kumhifadhi.
“Siku ya pili baada ya Lissu kupelekwa Nairobi, dereva wake aliletwa sababu siku ya tukio makamanda wa Chadema Dodoma walimhifadhi na baadaye tulimpeleka Nairobi kupata matibabu ya kisaikolojia kwa kuwa alikuwa mtu wa kwanza kushuhudia damu ya Lissu ikimwagika,” alisema.
Kauli kwa familia
Muro alisema mdogo wake hakuwa mwepesi wa kuzungumza yanayomkabili, lakini kuna siku alizungumza kauli yenye utata ambayo amekuwa akiifikiria.
Alisema akikariri maneno ya Lissu, “Kuna wakati nafikiria tupo kwenye tanuru la moto wa mkaa wa tofali kama unaweza kutokea huku na huku tanuru linawaka ni kazi ngumu mbele yangu, kama nakanyaga tanuru nitokee upande wa pili.”
Muro alisema hakumjibu lakini alishangaa ni kwa nini alitoa kauli hiyo.
Alisema japokuwa familia ilikuwa inaona anachokifanya ni kizuri, lakini yeye Muro kuna wakati alikuwa akiwaza.
Muro alisema wiki mbili kabla ya tukio hilo, Lissu alikutana na familia yake alipohudhuria mazishi ya kaka yao na kwa kipindi chote walichokaa naye hakusema lolote.
“Baada ya kukutana, tumekaa, tumezika mpaka tukafanya kikao jioni cha ukoo kwa kweli hakuzungumza lolote na tangu alipotoka huku hatujawasiliana naye,” alisema.
Shambulio la risasi
Muro alisema tukio la Lissu kushambuliwa lilimshtua kila mwanafamilia na mpaka sasa hawajui cha kufanya na zaidi ya kusubiri taarifa kutoka kwa vyombo vya ulinzi na usalama.
“Mimi nafanya kazi pale Ikungi, siku hiyo nilikuwa nimepumzika saa saba hivi watoto wakaja mbio wakaniambia baba; baba mdogo kapigwa risasi niliruka sababu nilikuwa usingizini, sentensi ya kwanza ilikuwa amekufa? Walinijibu subiri kidogo,” alisema.
Muro alisema alipoambiwa kuwa amepelekwa hospitali Dodoma alipumzika kwa nusu saa baadaye akaamua kuelekea huko.
“Nilipofika Manyoni nilipigiwa simu kuambiwa nirudi maana hata ningefika nisingeweza kumuona kwa kuwa wanafanya utaratibu wa kwenda Nairobi, Nilirudia hapo. Familia tumepigwa na mshangao na mpaka sasa japokuwa tunasikia kwamba hali yake ni nafuu lakini tumelipokea suala hili kwa mshtuko mkubwa ,” alisema.
Alisema baba yake mdogo, shangazi zake, mama zake wadogo, binamu zake na hata wapigakura wake wa Ikungi na wananchi kwa jumla walipigwa na bumbuazi.
Muro alisema familia imewatuma ndugu akiwamo kaka yake Alute ambaye ni mwanasheria jijini Arusha, mjomba wao na dada yao anayeishi Songea kwenda Nairobi kufuatilia hali yake.
“Kule kuna dereva wake ambaye yupo karibu na sisi, mke wake na watu wengine ambao ni viongozi wa chama wapo kule. Kuna dada yetu anayekaa Songea na kesho anaondoka mdogo wetu anaitwa Vincent, ni muda mfupi hatujafikiria tufanye nini,” alisema.
Muro alisema mwishoni mwa mwezi huu watafanya kikao Dar es Salaam wajue nini cha kufanya.
Baba mdogo wa Lissu, Muro Sawa (79), alisema kitu ambacho wazazi wangefurahia ni kumwona kijana wao akirudi nyumbani akiwa mzima.
“Familia tutakaa kikao kushauriana ili tujue suala hili tunalitatua vipi, lakini niiombe Serikali kumzidishia ulinzi kijana wangu. Sisi familia tuna uchungu mkubwa kuhusu hili,” alisema Sawa.
Shangazi wa Lissu, Ninaa Sawa Muro (83) alisema, “Tunakula chakula hakishuki, matonge yanakaba shingoni, maungo yote yanauma kwa sababu ya mtoto wetu, tangu siku ile niliposikia nilikuwa kwenye kiti ghafla nikaanguka na kuanza kutetemeka.”
Alisema alijisikia vibaya baada ya kuambiwa na mtoto wake taarifa hizo, “Aliniuliza umesikia kwamba Tundu Lissu amepigwa risasi? Nikanyamaza, nikaona joto. Kwa jinsi shangazi yangu anavyonipenda hata anikute Manyoni hata Dar es Salaam ananiita jina langu la kikwetu anakuja ananikumbatia iliniuma sana.”
“Alifanywa hivyo kwa nini? Kama tunavyojiona wote roho moja tumfikirie huyo Tundu Lissu,” alisema shangazi huyo ambaye baada ya baba yake Lissu kuzaliwa ndiye aliyemfuata.
Mama mdogo wa Lissu, Bula Muro, alisema baada ya kupata taarifa alianguka chini na kuanza kulia hakufikiria kama amepona.
Mitandao ilivyoiliza familia
Mmoja wa wanafamilia, Msengi Ntandu Mughwai alisema walipata shida siku hiyo ya tukio, “Tulipanga kwenda Dodoma wakasema turudi anaendelea na matibabu, tulihisi wanatudanganya sababu mtandaoni wanasema hali mbaya na kwa kuwa walikuwa ni wanafamilia waliotushauri, tuliamua kurudi usiku kwa kweli kesho yake kulikuwa na habari za ajabu kwenye mitandao yaani zilituumiza sana,” alisema.
Msengi alisema walikuwa wakipigiwa simu na kupewa taarifa zenye utata na wakiingia mitandaoni wanaona habari za ajabuajabu na kwamba hali kwao ilikuwa mbaya.
“Kwa kweli tulipata shida, wazazi wetu walikuwa wanakuja mara kwa mara tunawajibu kwamba anaendelea vizuri lakini wazee wetu walikuwa wanapata taarifa mbaya kwingine kutokana na mitandao ya kijamii,” alisema.
No comments