FAHAMU UTARATIBU MPYA WA MUHIMBILI
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeanzisha utaratibu maalumu wa taarifa za nje kwa wagonjwa na ndugu wanaofika hospitalini hapo.
Hatua hiyo imeelezwa inalenga kupambana na ‘vishoka’ wakiwemo madaktari feki.
Utaratibu huo unahusisha wahudumu katika maeneo mkakati ambao wanavaa vizibao vya kijani vyenye maneno ‘Ask Me’ upande wa nyuma na mbele yakisomeka ‘Niulize Mimi’ ili inapotokea mtu anataka kuuliza ahudumiwe kwa urahisi na kupata maelekezo kwa usahihi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma Muhimbili, Aminiel Aligaesha amesema wana eneo kubwa la kutoa huduma, hivyo wateja wamekuwa wakihangaika wanapofika hospitalini hapo na matokeo yake wengine huishia mikononi mwa vishoka.
“Tumeweka utaratibu maalumu wa ‘Niulize Mimi” mahsusi kwa ajili ya kuwaelekeza watu mahali pa kwenda, hii itasaidia kuwaondolea usumbufu wateja na kuondoa vishoka, wakiwemo madaktari feki,” amesema.
Aligaesha amesema wanasikiliza pia maoni na malalamiko ya wateja na kuyatafutia ufumbuzi.
“Ikumbukwe pia, hapa Muhimbili tuna taasisi nne na wateja walikuwa wanachanganya taasisi hizo hivyo kuwaweka watu hao ni kuhakikisha mteja anapata kile anachokitaka kwa wakati,” amesema.
No comments