CHIRWA; NITAWANYOOSHA MAJIMAJI SONGEA
OBBREY CHIRWA.
MSHAMBULIAJI wa Yanga aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu, Obbrey Chirwa, amesema kwa sasa yupo fiti kuitumikia timu yake na ametoa onyo kwa wapinzani wao wa Jumamosi, Majimaji ya Songea.
Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa, itaumana na wenyeji wao hao kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea baada ya Jumapili iliyopita kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Njombe Mji ya Njombe huku Chirwa akicheza kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa ligi kutokana na kuwa majeruhi.
Akizungumza na gazeti hili kutoka kwenye kambi ya timu hiyo mkoani Njombe, Chirwa, alisema anajisikia kupona kabisa na kama atapewa nafasi ya kucheza mchezo ujao, atahakikisha anaisaidia timu yake kupata ushindi.
"Sio lazima nifunge mimi, nataka kuona timu yangu inapata ushindi, haijalishi nani atafunga, nimetoka kwenye majeruhi, lakini nina ari ya kupambana," alisema Chirwa ambaye mchezo uliopita alicheza kwa dakika 37 akiingia kipindi cha pili.
Alisema anajituma katika mazoezi kuhakikisha anarejea katika kiwango chake cha juu kama ilivyokuwa msimu uliopita ambao alikuwa na mchango mkubwa kwa timu yake mpaka kufanikiwa kutwaa ubingwa wa tatu mfululizo.
Kikosi hicho cha Yanga kinaondoka leo mkoani Njombe kuelekea Songea tayari kwa mchezo huo wa Jumamosi unaotegemewa kuwa wa upinzani mkubwa.
No comments