ACT WAZALENDO KIMELAANI KUSHAMBULIWA KWA RISASI KWA MEJA JENERALI MSTAAFU
Chama cha ACT Wazalendo kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kushambuliwa kwa risasi na kujeruhiwa kwa Meja Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) Vicent Mritaba kulikofanywa na ‘’Watu Wasiojulikana’’.
Kabla ya kustaafu, Meja Jenerali Vicent Mritaba amewahi kuwa Mkuu wa Utumishi wa JWTZ. Akiwa kwenye nafasi hiyo, atakumbukwa kwa msisitizo wake kwa wanajeshi kujiepusha na vitendo viovu hasa kuwapiga raia na kujichukulia sheria mkononi ambavyo vinakwenda kinyume na wajibu wa JWTZ wa kulinda mipaka ya nchi, raia na mali zao na kushiriki kazi za kijamii.
Pia, Chama chetu kinalaani vikali uvamizi wa ofisi ya Mawakili ya Prime Attorneys uliofanyika usiku wa kuamkia leo Jumanne 12 Septemba, 2017 jijini Dar es salaam.
Kuwepo kwa taarifa kwamba, pamoja na mambo mengine, wahalifu hao waliiba kasiki lenye nyaraka mbalimbali za ofisi ni dalili ya wazi kwamba hawakuwa wahalifu wa kawaida.
Vitendo hivi vya kuvamia na kuharibu ofisi za mawakili ambavyo vimetamalaki hivi sasa, bila shaka vinatishia uhuru wa mawakili katika utekelezaji wajibu wao kama Maafisa wa Mahakama.
Chama cha ACT kinalaani matukio yote haya mawili na kuvitaka vyombo vya dola hasa Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi la Polisi kuyachunguza matukio haya kwa umakini na kuhakikisha watekelezaji wake wanafikishwa kwenye mkono wa sheria.
Matukio ya kuvamiwa watu na kupigwa risasi yamekuwa yakiripotiwa siku za hivi karibuni ambapo September 7, 2017 liliripotiwa tukio la kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kabla ya September 11, 2017 kuripotiwa kushambuliwa Meja Jenerali Mstaafu Vicent Mritaba wakati anaingia getini nyumbani kwake.
Matukio haya yamekuwa yakikemewa na watu mbalimbali na viongozi wa kisiasa, dini, Taasisi na Serikali na kufuatia tukio la September 11 la kupigwa risasa kwa Meja Jenerali Mstaafu Vicent Mritaba Chama cha ACT Wazalendo kupitia kwa Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi, Ado
Shaibu jana September 12, 2017 kilitoa tamko kulaani.
Ado Shaibu,
Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi
ACT Wazalendo.
No comments