Breaking News

IGP SIRRO AFANYA ZIARA YA KUSHITUKIZA STENDI KUU YA MABASI UBUNGO

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amewataka madereva na wamiliki wa mabasi ya abiria yaendayo mikoani na nchi jirani pamoja na wamiliki na madereva wa mabasi madogo ya abiria maarufu kama daladala kuhakikisha wanayafanyia ukaguzi na matengenezo ya mara kwa mara magari yao ili kupunguza ajali zinazosababishwa na ubovu na uchakavu wa magari.

IGP Sirro aliyasema hayo jana wakati alipofanya ukaguzi wa kushtukiza katika Kituo Kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani pamoja na kituo cha daladala cha Mbezi Luisi kwa lengo la kuangalia hali ya usalama wa kituo hicho, kuona namna ukaguzi wa mabasi ya abiria unavyofanyika kabla hayajaanza pamoja na kusikiliza kero mbalimbali za abiria.

“Nimefarijika kuona watendaji wa kituo hiki pamoja na askari wangu wakifanya kazi vizuri kwa ushirikiano mkubwa hali inayosaidia kupunguza kero mbalimbali kwa watumiaji wa kituo hiki” alisema IGP Sirro.

Aliongeza kuwa Ubungo ni salama na itaendelea kuwa salama kwa sababu vibaka wamepungua na wale wanaofanya utapeli katika kituo hicho waache mara moja na kutafuta kazi nyingine kwa kuwa mwisho wa siku wataacha familia zao baada ya kukumbana na mkono wa sheria.

Pia ameelekeza magari yote ya abiria yabandikwe namba simu zote za makamanda wa mikoa wa Kikosi cha Usalama Barabarani pamoja na Wakuu wa Polisi wa wilaya zote sehemu ambazo itakuwa ni rahisi kuonekana na abiria ili iwe rahisi kwao kutoa taarifa pindi wanapoona dereva anaendesha gari kwa kukiuka sheria na kanuni za usalama barabarani.

Aliwataka wananchi kuendelae kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ikiwa ni pamoja kutii sheria bila shuruti na kutoa wito kwa wamiliki wa magari, madereva pamoja na abiria kuwa wastaabu na kuhakikisha wanaheshimu sheria na kanuni za usalama barabarani kwa kuwa kila mmoja anafahamu madhara ya ajali.

No comments