Watu 18 wajeruhiwa ajalini Dar
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni
WATU 18 wamejeruhiwa katika ajali iliyotokea saa 10:30 alfajiri katika eneo la Madafu barabara ya Pugu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamdani alisema ajali hiyo ilihusisha gari namba T 337 BKN Nissan Civilian iliyokuwa inatoka Gongo la Mboto – Mombasa kwenda Kariakoo kupitia Banana.
“Gari hilo liliigonga gari la mchanga namba T 656 DHL Scania 94 lililokuwa likitokea Banana kwenda Gongo la Mboto,.
“Watu 18 walijeruhiwa katika ajali hiyo na kupelekwa katika Hospitali ya Amana wakati wengine walipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Hali za majeruhi watatu zilikuwa mbaya,” alisema.
Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Neema Mwangomo alithibitisha hospitali hiyo ilipokea majeruhi tisa na mwili mmoja wa marehemu.
Mwangomo aliwataja majeruhi waliopokelewa hospitalini hapo kuwa ni Masiku Werema (45), Mohamed Juma (37), Adam Rashid (25) na Joshua Stephen (32).
Wengine ni Said Juma (17), Eliza Chacha (14), Maua Malick (48), Stella Mpahe (35) na Juma Mtally.
“Kati ya majeruhi hao, Adam Rashid alipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya hali yake kutengamaa,” alisema.
Mwangomo alisema majeruhi wengine bado wamelazwa wakiendelea kupatiwa matibabu.
No comments