Taifa Stars kukipiga na Afrika Kusini kesho
Dar es Salaam. Taifa Stars itashuka uwanjani kesho Jumapili Julai 2, kuivaa Afrika Kusini Bafana Bafana katika mchezo wa robo fainali ya mashindano ya Cosafa utakaofanyika kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng, (saa 12:00 jioni kwa saa za Tanzania).
Stars itaingia katika mchezo huo ikiwa na rekodi nzuri ya hatua ya makundi kwa kufungwa bao 1 katika mechi tatu baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mauritius, na kutoka suluhu na Angalo na kushinda 2-0 dhidi ya Malawi.
Kocha Salum Mayanga, amesema anabadili mbinu za kuivaa Afrika Kusini, kesho Jumapili.
Kocha Mayanga, alisema ili kufanikiwa dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Cosafa 'Bafana Bafana' watalazimika kutumia mbinu tofauti na ilivyokuwa katika mechi za makundi.
"Kwanza tunashukuru Mungu, hapa tulipofikia haikuwa rahisi, maana tulianza kwa kuwafunga Malawi mabao 2-0, kupitia kwa Shiza Kichuya, tukatoka sare tasa na Angola, tumetoka sare ya bao 1-1 na Mauritius, bao hilo lilifungwa na Simon Msuva,"alisema Mayanga.
Bafana Bafana itawakosa nyota wake wa kikosi cha kwanza katika mchezo huo, lakini kocha wao mpya Stuart Baxter anaamini vijana aliowachagua ni hatua nzuri katika kutegeneza kikosi kipana cha timu ya taifa kwa siku za mbeleni.
“Tumechagua timu ya kushiriki Cosafa tukiwa na vijana wenye wastani wa umri wa miaka 22.6, na wengini ni vijana kutoka katika timu ya taifa ya U20 iliyoshiriki Kombe la Dunia Korea,” alifafanua Baxter.
Afrika Kusini na Tanzania zimekutana mara mbili zote zikiwa ni mechi za kirafiki: Mara ya kwanza zilikutana Dar es Salaam Oktoba 2002 na kutoka sare 1-1 na kurudiana tena Dar es Salaam Mei 2011 na Bafana Bafana kushinda kwa bao 1-0.
No comments