Sakaya awekwa mtegoni CCM, CUF
Rais John Magufuli akihutubia wananchi wa Kijiji cha Luchugi-Uvinza, Kigoma jana akiwa njiani kuelekea Tabora kuanza ziara ya kiserikali mkoani humo. Picha na Ikulu
Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, alisema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Kaliua, Tabora wakati wa ufunguzi wa Barabara ya Kaliua – Kazilambwa, kwenye Uwanja wa Kasungu.
Rais John Magufuli ni kama amemuweka katika mtego Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya baada ya kumpongeza kwa ushirikiano wake katika shughuli za maendeleo huku akisema ingawa kimwili mbunge huyo ni wa CUF, lakini damu yake na roho yake ni vya CCM.
Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, alisema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Kaliua, Tabora wakati wa ufunguzi wa Barabara ya Kaliua – Kazilambwa, kwenye Uwanja wa Kasungu.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 56, imejengwa kwa kiwango cha lami kwa zaidi ya Sh61.86 bilioni, zote zikiwa ni fedha za ndani.
Akimzungumzia Sakaya ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Rais Magufuli alisema amekuwa akifanya kazi nzuri za maendeleo katika kutekeleza ilani ya CCM, huku akimtaka kuendelea kuwapa maendeleo wananchi bila kuwabagua kwa itikadi ya vyama vyao na akawataka wanaCCM kushirikiana naye. Alisema kuwa ni bora kuwa na wanachama wa chama kingine anayefanya kazi za CCM kuliko kuwa na mwana-CCM anayefanya kazi za vyama vingine.
“Mheshimiwa Sakaya ukimwangalia mwili wake ni mwana-CUF, lakini damu yake na roho yake ni mwana CCM. Inawezekana siku moja akahamia CCM. Ni bora kuwa na mwanaCUF, au mwana Chadema, au mwana-ACT anayefanya kazi za CCM kuliko kuwa na mwana CCM anayefanya kazi za chama kingine. Si mmenielewa? Mimi najua maana hata wakati wa kampeni niliyaona.”
Awali, akitoa salaam zake kwa niaba ya wananchi wa Kaliua, Sakaya alimpongeza Rais Magufuli na kumhakikishia kuwa anamuunga mkono kwa juhudi zake za kuwatetea Watanzania na kuwaletea maendeleo akisema barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa wananchi wa jimbo lake ambao alisema asilimia 85 ni wakulima.
Pia, alimuomba awaongezee kilomita nyingine za lami pamoja na huduma ya maji aliyosema ni tatizo kubwa, ili Kaliua ipige hatua za maendeleo haraka.
Katika hotuba yake, Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuongeza barabara nyingine zenye jumla ya urefu wa kilomita 112 akisema fedha si tatizo.
Hizo ni pamoja na barabara ya Kahama - Urambo ya kilomita 28 ambayo mchakato wake wa ujenzi unaanza ndani ya mwezi na Chanya -Nyaua ya kilomita 84 ambayo nayo mchakato wake ni ndani ya siku 45.
Pia Rais Magufuli ameziagiza mamlaka zinazohusika na ujenzi wa reli ya kisasa, kuanza kubomoa nyumba za wanaCCM waliojenga kwenye hifadhi ya reli hiyo zao huku akisema kuwa sheria ni msumeno.
Aliwataka pia waliojenga kandokando ya reli hiyo kujiandaa kisaikolojia kwa kuwa zote zitaondolewa. “Kuna baadhi ya watu tena wengine ni wanaCCM wanaopitapita na kusema kuwa hazitabomolewa, ukifika wakati anzeni na za wana-CCM. Mimi ndio mwenyekiti wa CCM, lakini sheria ni msumeno,” alisema.
Kuhusu mazingira, Rais Magufuli alisema Mkoa wa Tabora ulikuwa na sifa ya kuyahifadhi lakini sasa nao umeanza kuingiliwa na ugonjwa ulioikumba mikoa mingine wa kufyeka miti na misitu ovyo.
Alisema wanaofanya uharibifu huo ni watu kutoka mikoa mingine na kwamba wengine walikaribishwa na kuruhusiwa na baadhi ya wana CCM kukaa kwenye maeneo ya hifadhi na kuwataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini kote kusimamia sheria katika kulinda mazingira na maeneo ya hifadhi.
No comments