IGP SIRRO KULIFUMUA JESHI LA POLISI KIMYA KIMYA
SIKU chache baada ya kuhamishwa aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Naibu Kamishna wa Polisi, Mohamed Mpinga, imefahamika kuwa mkuu wa jeshi hilo, IGP Simon Sirro
anaendelea na panga pangua ambayo imewaondoa maofisa zaidi ya 100 kutoka Makao Makuu jijini Dar es Salaam kwenda kufanya kazi chini ya makamanda wa mikoa.
Naibu Kamishna Mpinga aliteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, na sasa imebainika kuwa IGP ataendeleza zoezi hilo ambalo lengo lake ni kuboresha utendaji wa jeshi hilo ili kufikia lengo la kuhakikisha ulinzi wa raia na mali zao.
Taarifa ambazo Gazeti la Nipashe imezipata kupitia chanzo chake cha uhakika ndani ya jeshi hilo, zilidai kwamba hadi sasa, ikiwa ni chini kidogo ya miezi miwili tangu Sirro aapishwe kuwa IGP, maofisa zaidi ya 100 wameshaondolewa kutoka Makao Makuu ya Polisi na kwenda katika maeneo mbalimbali nchini ili kuimarisha utendaji wa jeshi hilo.
"Kuna uhamisho mkubwa wa kimyakimya unaoendelea kila siku ndani ya jeshi," kilisema chanzo hicho cha habari na kwamba "lengo ni kuimarisha utendaji."
"Isipokuwa wengi waliokumbwa na uhamisho huu ni maofisa waliokuwa makao makuu ambao kwa kiasi fulani ujuzi wao ulikuwa hautumiki vizuri kwa manufaa ya taifa.
"Kuna watu wana ujuzi wa hali ya juu unaohitajika na jeshi, lakini walikuwa wapo tu pale makao makuu. Wengi kati yao wameguswa na panga pangua hii."
Alipoulizwa na Nipashe kuhusiana na ukweli wa taarifa hiyo, Msemaji wa Polisi, Kamishna Msaidizi Barnabas Mwakalukwa, ambaye naye ni zao la mabadiliko yanayoendelea ndani ya jeshi hilo baada ya kuchukua nafasi ya Advera Bulimba aliyehamishiwa Mwanza, alisema uhamisho wa askari kutoka eneo moja kwenda jingine ni jambo la kawaida.
Katika mabadiliko hayo, nafasi ya Mpinga imechukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Fortunatus Musilimu.
Habari hizo ziliiambia Nipashe kwamba maofisa hao wamepelekwa kwenye vituo ili wakafanye kazi za kipolisi zaidi kuliko kushinda Makao Makuu ambako walionekana kama hawatumiki ipasavyo.
"Maofisi na askari wameondolewa na wengi wao wamepelekwa kwenye mkoa wa kipolisi wa Ilala na Temeke kufanya shughuli za kipolisi zaidi na kuwabakiza watu wachache hapa makao makuu kwa ajili ya shughuli za kisera zaidi," chanzo hicho kilieleza.
Kilisema zaidi:"Idadi kamili ya walioondolewa sijaipata kwa kuwa kila mara inakuja orodha tofauti.
"Kuna siku unasikia watu 20 siku nyinyine idadi inakuja tofauti ila ni wengi walioondolewa makao makuu na huenda wakafika hata 200."
NDANI KWA NDANI
Akifafanua zaidi kuhusu taarifa hizo, Kamishna Msaidizi Mwakalukwa alisema kuwa wanaendelea na uhamisho wao wa ndani kwa ndani.
"Hiyo taarifa sina. Mabadailiko nilishayatoa kwa vyombo vya habari. Hakuna mabadiliko mengine... sisi tunaendelea na kazi zetu na uhamisho wetu wa ndani kwa ndani unaendelea," alisema Mwakalukwa.
"Nitatoa kitu ambacho kimefika katika dawati langu, nitazungumza kama Msemaji wa Jeshi... lakini kama hakijafika siwezi kusema lolote kuhusiana na mfumo wetu," alisema.
Alisema suala la uhamisho lipo siku nyingi na linaendelea na askari hawatakiwi kukaa kituo kimoja kwa muda mrefu bali kubadilishana kazi na kupata uzoefu.
"Polisi kazi zetu zilivyo, kwanza wanapanda vyeo... na askari akipanda cheo inamaanisha apewe sehemu ambayo inalingana na cheo chake," alisema.
Alisema polisi huwa na operesheni mbalimbali zinazowalazimu askari kutokaa eneo moja.
"Mara utasikia leo utakwenda Manzense, mara Kigamboni... sasa sijui huo nao utaita ni uhamisho? Ina maana magazeti yenu mtaandika leo (askari) ameenda Magomeni, mara Kinondoni?"
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam wa zamani IGP Sirro aliteuliwa kushika nafasi ya mtangulizi wake, Ernest Mangu Mei 28, mwaka huu na kuapishwa siku moja baadaye.
Baada ya kuapishwa kuwa IGP mpya na kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, Sirro alisema kipaumbele chake cha kwanza ni kuzuia na kupambana na uhalifu na kuhakikisha nidhamu kwa watendaji ndani ya Jeshi hilo inakuwapo muda wote.
Kabla ya uteuzi wa IGP Sirro watangulizi wake tangu mwaka 1961 ni Elewangwa Shahidi, Hamza Aziz, Samwel Pundugu, Philemon Mgaya, Solomon Liani, Haroun Mahundi, Omar Mahita, Said Mwema na Mangu.
No comments