Hii ndio simulizi ya maisha ya Ebitoke
KOMEDIANI wa kike Bongo, Anastazia Exavery ‘Ebitoke’ (19) anayefanya vizuri zaidi kupitia mitandao ya kijamii alipitia mambo mengi ikiwemo kufanya kazi za ndani ‘house girl’ huku dada yake akiwa kikwazo cha yeye kutoboa kisanaa. Showbiz Xtra imefanya mahojiano maalum na Ebitoke kuhusu maisha yake kabla na baada ya kuwa staa.
MAISHA YAKE
Ebitoke anafunguka: “Mimi ni Mkerewe ila nimezaliwa Kijiji cha Kiuwani Wilaya ya MulebaVijijini mkoani Kagera.
ELIMU YAKE
“Nilianza darasa la kwanza mwaka 2006 ambapo nilimaliza darasa la saba mwaka 2013 katika Shule ya Msingi Kalema iliyoko Chato mkoani Geita. Baada ya kumaliza shule ya msingi sikufanikiwa kuendelea na masomo hivyo nikajikuta nikiwa sina hili wala lile pale kijijini kwetu.
UGUMU WA MAISHA WAMTIMSHA
“Nilipoona maisha yanazidi kuwa magumu pale kijijini, nilikimbilia jijini Mwanza kwa ajili ya kutafuta kazi za ndani, nilifanikiwa kupata kazi nikiwa na dada yangu.
ALIVYOFIKA DAR
“Nilifanya kazi zile za ndani kwa muda, baadaye mjomba wangu ambaye anaishi MbeziBeach (Dar), aliniita Dar ili nimsaidie kulea watoto wake na huo ndiyo ukawa mwanzo wa kulijua Jiji la Dar nikiamini huko ndiko ndoto yangu ya kuwa mwigizaji ingetimia.
ASEPA KWA MJOMBA’KE
“Baada ya kuona siwezi kutimiza ndoto zangu za kuigiza nikiwa kwa mjomba, mwaka 2015, niliondoka kwa mjomba na kwenda kwa rafiki yangu mmoja kule Kibaha, Pwani.
MAISHA YAMCHAPA, AKUMBUKA KWA MJOMBA
“Nikiwa kwa rafiki yangu, maisha yalinichapa sana kutokana na kuwa magumu kiasi cha kunifanya nikumbuke kwa mjomba. Ukizingatia sikufukuzwa wala sikuondoka kwa mabaya bali kwa lengo la kufikia malengo yangu.
AANZA KUUZA MGAHAWA
“Kutokana na ugumu wa maisha, nilianza kufanya kazi kwenye mgahawa kama Mama-lishe ili niweze kujikimu na kuepuka vishawishi vya hapa na pale.
ATAFUTIWA KAZI ZA NDANI TENA
“Nilifanikiwa kupata rafiki mwingine kule Kibaha aliyenitafutia kazi za ndani maeneo ya Mikocheni (Dar) ambapo nikafanya kazi miezi sita.
APATA SIMU NA KUJIUNGA MITANDAONI
“Baada ya kufanya kazi kwa muda, nilipata simu ya kisasa ambayo niliweza kujiunga kwenye mitandao ya kijamii.
AKUTANA NA TANGAZO
“Nikiwa naperuzi kwenye mitandao ya kijamii, nilikutana na tangazo kuwa Kampuni ya Timamu African Media inahitaji wasanii. Nikaamua kuomba nafasi, nikaitwa kwenye usaili, nikapita.
AAMSHA DUDE KWA BOSI WAKE
“Niliposhinda usaili, nikawa ninatakiwa niende mazoezini, lakini ikawa ni ngumu kwa bosi wangu kunikubalia. Niliamua kuliamsha dude kwa kusudi ili nifukuzwe. Nikawa nikipewa kazi na bosi ninakataa, hapo ndipo nikafuzwa. Nilifanya vile ili nipate sehemu ambayo inaweza kunipa nafasi ya kwenda kufanya mazoezi.
AISHI GETO
“Baada ya kufukuzwa kwa yule bosi wa Mikocheni, nilikwenda Mabibo kwa dada yangu aliyekuwa anaishi geto na wasichana wenzake wanne. Maisha hayakuwa mazuri kwa sababu tulimtegemea mtu mmoja aliyekuwa anafanya biashara.
AZINGUANA NA DADA YAKE
“Pale kwa dada nilipata nafasi ya kufanya mazoezi, lakini dada yangu hakuwa anapenda. Alikuwa akinigombeza kila siku.
APATA KAZI BAA
“Nilipoona dada yangu hapendi niigize, niliamua kuhamia kwa rafiki yangu mwingine maeneo ya Tegeta (Dar) niliyekuwa ninaigiza naye. Alinitafutia kazi ya baa ambayo ilikuwa hainibani kwani nilipata nafasi ya kwenda kufanya mazoezi.
ALIVYOSHINDWA KAZI YA BAA
“Nilifanya kazi ya baa kwa miezi mitatu, nikaacha kwa sababu wanaume wengi walikuwa wananisumbua halafu wenzangu karibu wote walikuwa wanakwenda kwa mabwana zao. Nikaona ninaweza kushawishika.
KUWAPIKIA WAJENZI
“Niliondoka pale na kwenda kukaa kwa dada yangu kwenye nyumba nyingine ya mjomba. Nikapata kibarua cha kuwa ninawapikia wajenzi halafu wananilipa shilingi elfu tano kwa siku. Ilikuwa ni kazi ngumu sana kupika ugali wa watu 12.
APITA KWENYE USAILI TENA
“Baadaye Timamu Media walifanya usaili wa mtu ambaye anaweza kuigiza kishamba, nikafanikiwa kupita, kila mtu akasema ninaiweza vizuri nafasi hiyo.
APEWA JINA LA EBITOKE
“Nikiwa mazoezini bosi wangu wa Timamu African Media, Timoth Kachumia aliniona ninavyocheza, ikabidi anipe jina la Ebitoke.
SINI ZA USHAMBA ZAMSUMBUA
“Mwanzoni nilisumbuka sana kuzoea kwani kuvaa nguo zile za kishamba na kupaka mafuta mengi ilikuwa inanipa shida, lakini sasa nimezoea.
MASHABIKI WAMPOKEA
“Kilichonifanya niendelee kuipenda sini (kipande cha kuigiza) ya ushamba ni vile mashabiki walivyonipokea na kunikubali.
TIMAMU WAMPA NAFASI
“Kabla sijatoka, kampuni ilianza kuwatoa Mkali Wenu, Mama Ashura, Mjeshi kisha mimi ndiyo nafuata, hapo ndipo nikapata nafasi ya kuwa Ebitoke.
MAFANIKIO YAKE
“Sijapata mafanikio makubwa kihivyo kwa sababu ndiyo nimeanza, ila ninaweza kujihudumia baadhi ya vitu na nimefahamika. Mashabiki wangu wategemee mambo mazuri kutoka kwangu na kama kuna wadau na makampuni wanakaribishwa.
Kwa hakika maisha ya ebitoke yako kama yangu
ReplyDelete