DC Mbulu azindua kampeni ya kupima mimba wanafunzi
Katika kampeni hiyo, mkuu huyo wa wilaya amewataka wakuu wa shule na wakurugenzi kuwapima wanafunzi kila baada ya miezi mitatu.
Mbulu. Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga, amezindua kampeni ya kuwapima mimba wanafunzi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kuhakikisha hakuna wanafunzi wajawazito na waliozaa kuendelea na masomo katika mfumo wa kawaida.
Kampeni hiyo inayoitwa ‘Mbulu bila Mimba za wanafunzi inawezekana; tuwaache wasome,’ inalenga kuwafikia wasichana wote wenye uwezo wa kuzaa na kwamba itakuwa endelevu.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 25, Mofuga amesema kampeni hiyo itawasaidia kurejesha maadili kwa jamii kwa kuacha kufanya ngono na wanafunzi.
Mkuu huyo wa wilaya amewaagiza wakurugenzi na wakuu wa shule kuwapima wanafunzi kila baada ya miezi mitatu na kwamba watakaobainika watakuwa wamejifukuzisha shule wenyewe.
"Serikali haina mpango wa kusomesha wanafunzi wajawazito hivyo nawataka mabinti msikubali kudanganywa,”amesema.
Pia amewaonya walimu na wananchi wenye uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi kuacha mara moja kwani wakibainika watakwenda jela miaka 30 bila huruma.
Mofuga pia amewataka walimu wakuu kusimamia taaluma na nidhamu na kuwafichua wazazi wanaokwamisha maendeleo ya wanafunzi shuleni kwa kuwatuma kuchunga ng'ombe siku za shule au kufanya biashara pamoja na wazazi wanaoficha wahalifu wa mimba au kukubaliana kuwaozesha.
No comments