Serikali yabainisha Asilimia 60 ya bidhaa nchini hutoka nje
Dodoma. Tanzania inaagiza asilimia 60.6 ya bidhaa kutoka nje ikiwa ni kiwango kikubwa kuliko kile kinachouzwa nje ya nchi kwa mwaka.
Bidhaa nyingi zinazoagizwa kutoka nje zinatoka katika nchi za China, India, Japan, Kenya na Afrika Kusini. Bidhaa hizo ni pamoja na magari, vipuri, chuma na vyombo mbalimbali vya kielekroniki.
Hata hivyo, Tanzania inauza zaidi chai, mahindi, mbogamboga, dhahabu na shaba katika nchi za Kenya na Afrika Kusini.
Akiwasilisha hotuba ya hali ya uchumi bungeni mjini Dodoma leo, Alhamisi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema katika kipindi cha Januari mpaka Machi mwaka huu, mauzo ya bidhaa nje ya nchi yamefikia Dola za Marekani 2.2 bilioni.
Dk Mpango amesema uagizaji wa bidhaa nje ya nchi ulikuwa na thamani ya Dola za Marekani 2 bilioni huku akiba ya fedha za kigeni ikiwa ni Dola za Marekani 4 bilioni na thamani ya dola moja kwa shilingi ilikuwa ni Sh2,229 kufikia Machi mwaka huu.
“Akiba ya fedha za kigeni imesaidia utengamavu wa thamani ya shilingi. Mpaka kufikia Machi mwaka huu, dola moja ilikuwa na thamani ya Sh2,229,” amesema Dk Mpango.
No comments