Breaking News

Rais JPM afuturisha Pwani, atoa neno kwa Waislamu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana  tarehe 21 Juni, 2017 amefuturisha wananchi wa mkoa wa Pwani na kuwataka waumini wa dini ya Kiislam na madhehebu mengine kuendeleza umoja na mshikano uliopo kwa muda mrefu kwa lengo la kudumisha amani nchini. 

Mhe. Rais Magufuli alisema anaungana na waumini wa dini ya Kiislamu nchini katika kumi la mwisho la Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kuwaombea kumaliza kwa amani ibada ya Funga ya Ramadhani ikiwa ni kutekeleza nguzo ya nne kati ya nguzo tano ya dini ya kiislam. 

Alisema kwa mujibu wa dini ya Kiislamu ibada ya Funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni muhimu kwani ni njia sahihi ya kujirekebisha kuachana na matendo maovu yanayoweza kusababisha kutenda dhambi. 

‘’Ramadhani ni ibada muhimu kwa Waislaam kwani ndio mwezi ambao huchoma dhambi zao na kutenda matendo mema hivyo ni muhimu kwa ndugu Waislaam kuendeleza yote mema ambayo wanafanya katika kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani ikiwa ni pamoja na kuliombea Taifa.’’ 

Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Aboubakar Zubeir Ali alitaka wananchi wa Tanzania bila kujali itikadi za kidini kuendelea kuliombea Taifa ili lizidi kuendelea kuwa na amani. 

Nae Kaimu Sheikh wa mkoa wa Pwani Sheikh Hamisi Mtupa alimshukuru Rais Magufuli kwa ukarimu wake wa kuwaaandalia futari wananchi wa mkoa wa Pwani ikiwa ni pamoja na makundi maalum ya watoto yatima wa kituo cha Bulome Foundation cha mjini Kibaha mkoani Pwani. 

Jaffar Haniu 
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU 
Kibaha, Pwani

No comments