Breaking News

NDESAMBURO AMUIBUA DK. SLAA,AELEZA JINSI WALIVYOLALA CHINI KUJENGA CHADEMA



Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa amesema kuwa amesikitishwa sana na kifo cha Mzee Philemon Ndesamburo na kueleza jinsi walivyokijenga chama pamoja.

Dk. Slaa amesema kuwa licha ya Ndesamburo kuwa na utajiri mkubwa, lakini hakuuona kuwa ni kitu bali ni nyenzo ya kuwakomboa wananchi katika sekta mbalimbali.

Dk. Slaa ameitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tangu aliyekuwa Mbunge wa Moshi Mjini kwa miaka 15, Mzee Philemon Ndesamburo alipozikwa nyumbani kwake KDC Moshi baada ya kufariki wiki iliyopita alivyopata matatizo ghafla akiwa ofisini kwake.

Dk. Slaa ambaye sasa anaishi Toroto nchini Canada baada ya kujiuzulu wadhifa wake na kuachana na siasa tangu mwaka juzi, alisema kuwa ameshtushwa sana na kifo cha ghafla cha kiongozi huyo tegemeo. Alieleza kuwa licha ya wao kubaki na majonzi, lakini anaamini kazi ya Mungu haina makosa wala haihojiwa.

"Ni kweli nimefanya kazi na Ndesamburo, tumejenga CHADEMA kwa pamoja hasa kipindi cha mwaka 2003 hadi 2005 ambapo tulizunguka nchi nzima," alisema Dk. Slaa na kuongeza kuwa licha ya mazingira magumu waliyokutana naye kwenye harakati za kukitangaza chama hicho, Mzee Ndesamburo hakulalamika alipotakiwa kulala chini, lakini aliona hizo ni changamoto za kutafuta ukombozi.

Aidha, Dk. Slaa alisema kuwa Mzee Ndesamburo alikuwa msikivu na mwenye kuelewa na kuwa tayari kuwasaidia wengi kwa hali na mali kwani mara kadhaa alitoa mali zake kuwasaidia wagombea wa CHADEMA na hata yeye mwenyewe kwenda kuwapigia kampeni bila kujali umbali aliotakiwa kwenda.

Akizungumzia kifo chake, Dk. Slaa alisema kuwa kifo hicho ni cha kusikitisha kwa sababu alifariki ghafla, hakupata nafasi ya kuagana na ndugu jamaa na marafiki. 

"Wakati mwingine afadhai mtu akiugua mnajiandaa kisaikolojia, ila akifariki ghafla tu, huwa ni kazi ngumu kuipokea ile hali.Kazi kubwa iliyobaki kwa watanzania sasa ni kutekeleza yale yote ambayo Mzee Ndesamburo amewaachia huku tukimuombea Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi."

Dk. Slaa aliondoka nchini mwaka 2015 baada ya kujiuzulu wadhifa wake kufuatia chama chake kumpokea na kumpa nafasi ya kugombea urais, aliyekuwa kada nguli wa CCM, Edward Lowassa.

No comments