Breaking News

Mastaa Hawa Mitandao Ya Kijamii Imewanusuru!


DAR ES SALAAM: Kwenye maisha kuna baadhi ya watu ambao wakiwa wanapata kipato kidogo au kikubwa, huwa wanaridhika mapema na hali wanayokuwanayo bila kufikiria kesho itakuwaje huku wakibweteka wakati wana uwezo wa kuongeza kipato zaidi.

Kwa mastaa wa Kibongo, hali hiyo ipo kwani baada ya sanaa kuwa ngumu kutokana na kazi zao za muziki au filamu kuwa haziuzi kama zamani, wengi wao wamejikuta wakiamka usingizini na kuanza kujishughulisha na biashara mbalimbali ili kujinusuru na balaa la kufulia.

Baadhi ya mastaa hao wa kike siku hizi wamekuwa wakitumia vizuri mitandao ya kijamii kutangaza biashara zao na kujikuta wakiongeza vipato vyao na kuendesha maisha vizuri hivyo kuachana na utegemezi wa ‘mabwana’, tofauti na zamani ambapo waliitumia mitandao hiyo kwa mambo yasiyowaingizia kipato.

Katika makala haya tunaangalia mastaa ambao wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, You Tube na Twitter kupitia kurasa zao kufanya biashara na hivyo kumudu kuendesha maisha na kuishinda hali ngumu waliyonayo hivi sasa.

MWANAHERI AHMED

Staa huyu wa filamu amekuwa akijishughulisha na biashara ya madera, lipstiki na urembo mwingine wa wanawake. Mwanaheri anauza bidhaa hizo kwa njia ya mtandao kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo wateja humpigia simu na kumfuata nyumbani kwake au kuwapelekea moja kwa moja pale walipo.

NISHA

Kabla ya soko la filamu kudorora, Nisha alikuwa amejikita kwenye uigizaji akitengeneza filamu za kawaida na zile za vichekesho. Nisha alianza na biashara ya saluni lakini kwa sasa amegeukia biashara ya kuuza nguo za maharusi ambapo amefungua duka huku wateja wake wengi akiwapata kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

FROA MVUNGI

Baada ya kuona atakufa njaa endapo ataendelea kubweteka ilihali sanaa imedunda, msanii huyu wa filamu alijiingiza kwenye biashara ya dawa za kupunguza unene na nguo ambapo alikuwa akiuza kwa njia ya mtandao kwani alikuwa akiposti kwenye ukurasa wake wa Instagram, lakini kwa sasa amegeukia kwenye biashara ya saluni.

SHILOLE

Mwanamuziki huyu ambaye pia ni Mwigizaji, awali alianza na biashara ya kuuza pochi na nguo za kike. Baadaye akahamia kwenye biashara ya baa na sasa anafanya biashara ya chakula. Amekuwa akitumia kurasa zake kutangaza chakula anachouza ambapo ana vijana wa bodaboda ambao huwapelekea chakula wateja wanaohitaji huku wengi wao wakipatikana kwenye mitandao.

JACQUELINE WOLPER

Mwanadada huyu ambaye ni msanii wa filamu, baada ya kuona soko limedunda aliamua kufungua duka la nguo za aina mbalimbali za wanawake pamoja na viatu. Wolper amewahi kukiri kuwa wateja wake wengi huwa ni wa mitandaoni kwani anatangaza sana kwenye ukurasa wake wa Instagram ndiyo anaowategemea zaidi tofauti na

maduka ya watu wengine.

WASTARA JUMA

Mwanamama huyu ambaye ni staa wa filamu amekuwa akitumia vizuri kurasa zake ambapo anauza nguo mbalimbali huku akipokea oda za wateja wake na kuwapelekea bidhaa zake popote walipo. Licha ya soko la filamu kukwama, Wastara ameendelea na maisha ya kawaida na familia yake bila kutetereka.

No comments