Breaking News

Mamia wakamatwa maandamano ya kupinga serikali Urusi

Polisi wa kupambana na fujo nchini Urusi, wamewakamata na kuwazuilia mamia ya waandamanaji waliokuwa wakipinga madai ya ufisadi katika Serikali ya nchi hiyo. 

Maandamano makubwa mno yameshuhudiwa katika miji ya Moscow na St Petersburg, mahali ambapo maelfu ya waandamanaji walijitokeza, huku wengi wao wakipiga kelele kumlaani Rais Vladimir Putin. 

Polisi wamemtia mbaroni mwandalizi wa maandamano hayo Alexei Navalny ambaye ni mkosoaji wa serikali na kiongozi mkuu wa upinzani nchini Urusi, Kiongozi mkuu wa idara ya usalama nchini Urusi, alitaja maandamano hayo kama ya uchokozi. 

Wengi wa waandamanaji walifoka "Putin is a thief!" yaani "Putin ni mwizi" "Russia will be free" yaani "Urusi itakuwa huru!" 

Zaidi ya watu 600 wanadaiwa kukamatwa na kuzuiliwa na maafisa wa polisi wa kupambana na fujo katika mji mkuu Moscow, na wengine 300 wamekamatwa katika mji wa St Petersburg. 

Bw Navalny anatazamiwa kumpinga Rais wa Vladimir Putin katika kiti cha Urais kwenye uchaguzi mkuu mwaka ujao, Rais Putin hajatangaza rasmi iwapo atawania tena kiti hicho au la. 




No comments