Kocha Simba Ataja Kilichosababisha Wakatolewa Sportpesa Super Cup
Mashabiki wengi wa Simba, jana Jumanne walionekana kuwa na nyuso za huzuni baada ya timu yao kutolewa na Nakuru All Stars ya Kenya katika michuano ya SportsPesa Super Cup.
Mara baada ya mchezo huo ambao walitolewa kwa penalti5-4, Kocha wa Makipa wa Simba, Idd Salim alielezea sababu kubwa iliyofanya wakapoteza mchezo huo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo uliokuwa mgumu kwa timu zote ulimalizika kwa matokeo ya 0-0 katika dakika 90 za kawaida na hivyo kulazimika kwenda kwenye hatua hiyo ya matuta ambaoo mchezaji pekee wa Simba aliyekosa penalti ni Daniel Agyei ambaye ni kipa.
Kocha Idd Salim amesema sababu kubwa iliyofanya wakashindwa kupata ushindi ni uwepo wa wachezaji wengi wageni ambao hawajui aina ya uchezaji wa Simba.
“Unajua timu yetu iliyocheza imeundwa na wachezaji wengi wageni, hawajui aina ya uchezaji wetu, wachezaji wetu wengi wapo kwenye timu ya taifa na wengine wapo katika mapumziko.
“Pamoja na hivyo tumecheza vizuri, msimu ulikuwa mzuri na sasa kinachofuata ni kujiandaa kwa ajili ya msimu ujao,” alisema kocha huyo.
Alipoulizwa juu ya Agyei kukosa penalti, alisema: “Ni jambo la kawaida, linatokea kwa mchezaji yeyote.
“Tunashukuru wafadhili wa michuano hii SportPesa kwa kuwa ni mashindano mazuri na yanaunganisha nchi za Afrika Mashariki, nadhani siku zijazo wataongeza na timu kutoka Uganda.”
No comments