Kibiti: Askari mgambo auawa
Rufiji. Mkazi wa Kitongoji cha Kazamoyo, wilayani hapa, Erick Mwarabu (37) ameuawa kwa kupigwa risasi usiku akiwa nyumbani kwake.
Watu wa karibu katika eneo hilo wamesema marehemu huyo aliyekuwa askari mgambo alipigwa risasi tatu akiwa uvunguni mwa kitanda alikokuwa amejificha.
Mkazi mmoja wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Simon amesema watu hao wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walivunja mlango wa nyumba yake saa 9.00 usiku kisha kuingia ndani na kutekeleza mauaji hayo.
Simon amesema baada ya watu hao kuingia ndani walipitiliza moja kwa moja hadi kwenye chumba chake ambapo walimkuta mkewe marehemu na kumhoji alipo mumewe.
Amesema baada ya kuona mkewe hataji mahali alipo mumewe walianza kumtafuta ndani ya nyumba yake na kufanikiwa kumuona marehemu akiwa amejificha uvunguni mwa kitanda ndipo wakamfyetulia risasi na kuondoka.
Simon amesema baada ya kutekeleza mauaji hayo hawakuchukua kitu chochote.
Mganga mkuu wa kituo cha afya Ikwiriri, Dk Iddy Malinda amesema katika uchunguzi walioufanya walibaini marehemu alikuwa na majeraha matatu ya risasi katika maeneo tofauti ya mwili wake.
“Majeraha mawili yalikuwa kwenye ubavu wa kulia na moja kichwani,”amesema.
Dk Malinda amesema mwili huo tayari umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga amesema polisi wanaendelea kufuatilia tukio hilo.
No comments