Kauli ya Ndugai mgawanyo wa bajeti yapingwa vikali
Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumza alipokuwa akiongoza kikao cha Bunge la Bajeti mjini Dodoma.
Ndugai alitoa hoja hiyo juzi jioni wakati Bunge likisubiri matokeo ya kura za kupitisha bajeti ya mwaka 2017/18 ambayo ni ya Sh31.71 trilioni.
Tangu Serikali ifute matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge mwaka jana, televisheni zimekuwa zikionyesha kipindi cha maswali na majibu tu na yanapoisha, matangazo hukatwa.
Dodoma. Hoja za Spika Job Ndugai kuwa kupiga kura za kukataa kupitisha bajeti ni kutotaka kupata mgawo wa fedha za maendeleo imepingwa vikali na wadau na wabunge wakisema ikifanyiwa kazi inaweza kuligawa Taifa.
Ndugai alitoa hoja hiyo juzi jioni wakati Bunge likisubiri matokeo ya kura za kupitisha bajeti ya mwaka 2017/18 ambayo ni ya Sh31.71 trilioni.
Tangu Serikali ifute matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge mwaka jana, televisheni zimekuwa zikionyesha kipindi cha maswali na majibu tu na yanapoisha, matangazo hukatwa.
Lakini juzi, kipindi hicho cha kupiga kura kilionyeshwa moja kwa moja na televisheni na wakati wa kusubiri matokeo hayo, Ndugai alitumia fursa hiyo kueleza athari za kupiga kura ya kupinga bajeti.
Alianza kudokeza wakati mbunge wa Mlimba (Chadema), Suzan Kiwanga alipokosea kura yake kwa kusema “ndio” badala ya “hapana” kama wabunge wengine wa upinzani na baadaye kutaka kura yake ihesabiwe kuwa “hapana”.
Ndugai aliwatuliza wabunge wa CCM waliokuwa wakishangilia na baadaye kumhakikishia Kiwanga kuwa kura yake itahesabiwa kwa mujibu wa utashi wake.
“Waheshimiwa wabunge tusikilizane ndugu zangu, naomba tumuhakikishie Mheshimiwa Suzan Kiwanga pamoja na kwamba hana barabara hana nini, lakini kasema bajeti haitaki, Ni ‘hapana’ hapo andika,” alisema Ndugai.
“Kazi kwenu mawaziri.”
Baada ya kumaliza kupiga kura na kutambulisha wageni, Ndugai alisema badala ya kukaa kimya kusubiri matokeo, anakaribisha miongozo na kuanza na wabunge wa Chadema, Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) na Mwita Waitara (Ukonga).
Sugu alihoji mantiki ya kauli yake kuhusu kupiga kura ya kukataa bajeti. Na ndipo baada ya kusikiliza hoja zote alisema bajeti ya sasa ni shirikishi tofauti na zamani, kwa hiyo haistahili kupingwa kwa kuwa kuipinga ni kukataa maendeleo.
Lakini hoja zake zimepingwa vikali na wadau.
Mratibu wa mtandao wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali ya Dodoma (Ngowedo), Edward Mbogo, alisema kauli ya Spika inaligawa taifa vipande na kuondoa maana nzima ya demokrasia ambayo inaifanya Tanzania isifiwe duniani.
Mbogo alipinga kauli hiyo na kusema kama itatekelezwa, inasababisha maumivu kwa wananchi wa kawaida na si kwa wabunge pekee na taifa litajikuta likipoteza maendeleo.
Maoni kama hayo alikuwa nayo makamu mwenyekiti wa Chaumma, Kayumbo Kabutali aliyesema kauli ya spika ni ya kibaguzi na inalenga kuwarudisha Watanzania katika mfumo wa chama kimoja.
Kabutali alidai kuwa Bunge limeanza kumshinda Spika kwa kuwa anaonekana kukosa hoja za msingi na zenye mashiko kwa Watanzania jambo alilosema ni hatari katika siasa za vyama vingi.
Mwalimu mstaafu, Asheri Ngabo, alisema kauli ya spika ilipaswa kutolewa ufafanuzi na Waziri Mkuu wakati ule ule aliotangaza ili kuondoa sintofahamu na kwamba kuiacha hadi sasa ni kuharibu heshima ya Bunge na kusababisha mawaziri wasifanye kile kilichoelezwa.
Katika viwanja vya bunge kuliendelezwa hoja za kupinga kauli ya Spika baada ya wabunge watatu wa upinzani kupata nafasi juzi.
Jana, mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche alisema suala la kutopeleka maendeleo katika majimbo ya upinzani halina mashiko na badala yake kinachotengenezwa ni siasa.
Heche alisema hata kwa baadhi ya maeneo kama jimboni kwake, kuna madiwani ambao wanatokana na CCM lakini wakati wa bajeti ya halmashauri wamekuwa wakipigia kura za kuipinga.
“Hawa wanacheza na siasa, hivi hawajui kuwa kuna watu milioni sita ambao waliipigia kura Ukawa? Sasa kama ni hivyo, wasije kukusanya kodi katika majimbo yetu,” alisema Heche
Alisema lengo la kura ya hapana lilikuwa si kutaka maji wala umeme bali kupeleka ujumbe kwa Serikali kuwa hawakubaliani na mambo mengi na wako tayari kurudi kwenye uchaguzi.
Mbunge wa Konde Khatib Said Haji (CUF) alikwenda mbali zaidi akisema suala la kutopeleka maendeleo kwa wabunge walioikataa bajeti litapingwa dunia nzima hadi ukweli upatikane.
Haji alisema kwa vyovyote itakavyokuwa kama kauli za aina hiyo zikiachwa, zinaweza kuligawa Taifa na kutokea mambo kama yaliyotokea Sudan.
Kauli ya kuligawa Taifa pia ilitolewa na mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde aliyesema kauli hizo zitaligawa Taifa na linarudisha nyuma nchi.
Mbunge mwingine aliyezungumza juzi, Peter Msigwa (Iringa Mjini, Chadema), alisema suala hilo haliwezekani kwa kuwa wanachofanya wabunge ni kusimamia kodi wanazolipa wananchi waliowatuma.
Naye mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alisema kama Serikali haitaki mawazo mbadala, iwasilishe bungeni muswada wa kubadilisha Katiba ili nchi irejee kwenye mfumo wa chama kimoja.
Mbunge wa viti maalumu (CCM), Fatuma Taofiq, aliyehojiwa jana, aliunga mkono kauli ya wapinzani kutopelekewa maendeleo kwa madai haitakuwa na maana kuwapa kitu ambacho wamekikataa.
Taofiq alisema mpango wa kuandaa bajeti ulikuwa ni shirikishi tangu hatua za awali lakini kitendo cha kuipinga hatua za mwisho ni usaliti ambao unapaswa kukemewa.
Suala hilo liliibuka tena jana wakati Naibu Waziri wa Ujenzi, Edwin Ngonyani alipomwambia mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule kuwa minara itajengwa jimboni kwake, lakini akumbuke kuwa aliikataa bajeti ya Serikali.
Spika Ndugai aliwaeleza mawaziri wakati wa mijadala ya mapendekezo ya bajeti za wizara zao kuwa wasipeleke fedha za miradi majimbo ya upinzani kwa kuwa wanasusia upitishwaji wa bajeti hizo, kauli ambayo alikuwa akiirudia mara kwa mara.
Spika alisema uamuzi wa wabunge hao unatokana na mawazo ya wananchi waliowapigia kura, hivyo wanapopiga kura wajue wanapigia kura wananchi wao.
Wengine walioungana na Spika Ndugai juzi ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Jenista Mhagama na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene.
No comments