Iringa: Majambazi wajeruhi na kupora fedha na dhahabu katika mgodi
Kundi la watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wamevamia mgodi wa dhahabu wa wachimbaji wadogo katika kijiji cha Nyakavangala kilichopo katika tarafa ya Isimani wilayani Iringa na kupora fedha tasilimu kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 80 na gramu 400 za dhahabu huku wakiwajeruhi watu tisa.
Majeruhi wa tukio hilo la uporaji ambao baadhi yao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa wamesimulia tukio hilo lililotokea siku ya tarehe 9 mwezi huu majira ya saa moja jioni ambapo kundi hilo la watu walivamia mgodini hapo na kuanza kuwasaka watu waliowataja kwa majina na kuwalazimisha baadhi ya wachimbaji kuwaonesha walipo watu hao.
Baadhi ya majeruhi hao wameiomba serikali kujenga kituo cha polisi katika eneo hilo la mgodi ili kuimarisha usalama wakisema kuwa uporaji huo ulifanyika kwa muda mrefu huku kukiwa hakuna msaada wowote kutokana na eneo hilo kutokuwa na kituo cha polisi wala huduma ya mtandao wa simu hali iliyowafanya majambazi hao kufanya tukio hilo kwa muda wa zaidi ya saa kwakuwa walijua hawatabughudhiwa wala kufurushwa na vyombo vya usalama.
Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka waporaji hao tangu walipopata taarifa hizo hapo jana na kuongeza kuwa serikali inashirikiana na wachimbaji katika eneo hilo la Nyakavangala kuratibu ujenzi wa kituo cha polisi ili kudhibiti usalama wa eneo hilo huku muhudumu wa afya wa Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa Bi Gloria Mnyonge akielezea hali za majeruhi hao.
No comments