Askari Mgambo mwingine apigwa risasi kisogoni akivuna ufuta Rufiji
Askari Mgambo, Nurdin Kisinga (33) Mkazi wa Kijiji cha Umwe Kaskazini Ikwiriri, wilayani Rufiji mkoani Pwani amelazwa katika Hospital ya Mchukwi baada ya kupigwa risasi ya kisongoni.
Huyu ni mgambo pili kipigwa risasi ndani ya siku mbili baada ya Erick Mwarabu kuuawa juzi saa tisa usiku akiwa uvunguni mwa kitanda chake.
Tukio la leo Jumatano limetokea katika eneo la Ngomboloni lililopo katika Kijiji cha Umwe Kaskazini ikiwa ni takribani saa 19 tangu Mkuu wa Jeshi la Polisi(IGP), Simon Sirro kufanya mkutano wa mazungumzo na wazee wa wilaya za Kibiti na Rufiji ili kukomesha mauaji katika wilaya hizo.
Akielezea jinsi tukio hilo lilivyotokea, kaka wa majeruhi aliyejitambulisha kwa jina la Kisinga Athumani Kisinga akiwa katika Hospitali ya Mchukwi alisema ndugu yake alipigwa risasi akiwa shambani kwake.
Alisema Nurdin alikuwa akivuna ufuta wake shambani kwake ndipo watu ambao hawajajulikana idadi yao walimpiga risasi moja ya kisogoni na kutokomea kusikojulikana.
Kisinga alisema Nurdin alikuwa ameambatana na vijana wawili ambao ni watoto wake kuvuna ufuta huo.
Alisema mara baada ya kuanguka chini wadogo zake waliomba msaada kwa kupiga yowe na ndipo mtu mmoja alifika eneo la tukio na kumchukua kwa baiskeli hadi barabarani.
Alisema mara baada ya kufika barabarani alifanikiwa kubebwa kwa pikipiki hadi kituo cha Polisi Ikwiriri.
Alifafanua kuwa baada ya hapo alikimbizwa katika kitio cha Afya Ikwiriri ambapo alipatia huduma ya kwanza kituoni hapo na baadaye alipelekwa Mchukwi kwa matibabu zaidi.
Mganga wa zamu katika hospitali hiyo Emmanuel Humbi alisema wanampeleka kwenye chumba cha X Ray kwa ajili ya uchunguzi.
No comments