JESHI LA POLISI LAMTUNISHIA MISULI WAZIRI WA MAMBO YA NDANI MWIGULU NCHEMBA...PF3 NI LAZIMA
Ijumaa, May 19, 2017
Baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kutoa taarifa kupitia ukurasa wake wa Facebook kuwa kuanzia sasa majeruhi, mahututi asiyeweza kutoroka atatibiwa kwanza ndipo ashughulikie fomu ya polisi namba 3 (PF3), Jeshi la Polisi limetolea ufafanuzi zaidi wa taarifa hiyo.
Katika taarifa ya Waziri Nchemba alisema, “Tumeamua, majeruhi, mahututi asiyeweza kutoroka,na mtu mwenye majeraha yasiyo na utata wapewe matibabu kwanza bila PF3.”
Aliendelea kueleza zaidi kwamba, “Hatua za kufuata PF3 zianze mara moja wakati akiendelea kupewa matibabu, hii tunalenga kuokoa maisha yao kwanza. Utaratibu huu unajicho la karibu kutoka kwenye vyombo vyetu vya usalama ili kubaini ukweli jeraha la mhusika.”
Kwa upande wa Jeshi la Polisi kupitia kwa msemaji wake, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba-ACP ameeleza umma wa Watazania kwamba, fomu hiyo ni ya lazima kwa mtu yeyote aliyepata majereha kabla ya kutibiwa na itaendelea kutumika kwa mujibu wa sheria.
“Fomu ya Polisi namba 3 ijulikanayo kama PF.3 hutolewa kwa mtu baada ya Polisi kupata taarifa kutoka kwa mlalamikaji au muathirika kwa matukio yenye madhara mwilini, ajali au matukio yenye kuleta mashaka kuhusu vyanzo vyake kama vile kipigo, kujeruhi, ubakaji, kulawiti, kunywa sumu na mengineyo.
“Ieleweke wazi kwamba matumizi ya PF3 ni ya lazima na yanaendelea kama kawaida kwa mujibu wa sheria. Fomu hiyo inapaswa kutumika katika kila aina ya tukio tajwa hapo juu ili muathirika aweze kupata matibabu katika vitu vya afya na hatua za kiupelelezi kwa Jeshi la Polisi ziweze kuendelea.”
Aidha, ACP Bulimba aliongeza kuwa, “Katika mazingira mengine hali ya muathirika yaweza kuwa mbaya, hivyo huduma za kuokoa maisha (huduma ya kwanza) inaweza kuendelea kutolewa wakati watoa huduma wakiijulisha Polisi ili kuharakisha upatikanaji wa PF.3”
No comments