SERIKALI YATOA RAI KWA WANANCHI
Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wake wa Mambo ya Ndani ya Mhe. Mwigulu Nchemba ametoa rai kwa wananchi na viongozi kwa ujumla kuwafichua wahamiaji haramu haraka iwezekanavyo na wala wasisubiri mpaka wanapoguswa kwenye maslahi zao.
Mhe. Mwigulu Nchemba ameeleza hayo leo bungeni katika mkutano wa nane bunge la 11, wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalum Zubeda Hasani Sakuru alipotaka kusikia kauli ya serikali juu ya ongezeko la matukio ya ukamataji wa wakimbizi nchini.
"Tunatoa rai kwa wananchi wote pamoja na viongozi kutoa ushirikiano kuwafichua wahamiaji haramu walipo muda wowote na siyo tu mpaka pale mnapoona maslahi yenu binafsi yameguswa", amesema Mwigulu.
Aidha, Waziri Mwigulu amesema jambo kubwa wanalolifanyiakazi katika kipindi hiki ili kukabiliana na wahamiaji haramu na kuhakikisha wanaboresha kuweka uimara katika mipaka ya nchi.
"Jambo linalotusumbua sasa hivi ni kuhangaika na kukabiliana na wahamiaji haramu katika nchi yetu lakini utakuta wameshasaidiwa kupita kuanzia wanapotoka ikiwepo nchi ya Kenya lakini pia wanapokuwa wamemaliza Tanzania. kwa hiyo hilo ni moja ya jambo tunalopambana nalo katika kuhakikisha tunaziba mianya kwa utaratibu wa kushirikiana pamoja na kutumia sheria zinazo uwiana", amesisitiza Mwigulu.
Kwa upande mwingine, Waziri Mwigulu amesema jeshi la polisi pamoja magereza wamekuwa wakiwasaidia wahamiaji haramu ambao wanapitishwa katika mipaka ya nchi na malori jambo ambalo linapelekea watu hao kukosa nguvu na wengine kufa hivyo jeshi la polisi huwa wanawapa huduma za kwanza ili kuweza kunusuru uhai wao kama binadamu.

No comments