OXLADE-CHAMBERLAIN KUNA MABADILIKO YENYE MATUMAINI.
Goli lake la jana linaweza vema kuuelezea msimu wake Alex Oxlade-Chamberlain . Kuna kitu ameongeza kwenye mpira wake. Ndiyo! Huu ndio msimu wake bora zaidi akiwa amehusika kwenye mabao 10 ya Liverpool msimu huu kwenye mashindano yote. Amefunga 5 na kutoa assisti 5.
Kiuchezaji Oxlade-Chamberlain amebadilika na amekuwa na utofauti mkubwa na kule alikokuwa mwanzo. Oxlade- Chamberlain kwa sasa anacheza kwenye mazingira yenye ushindani kuliko aliyokuwa nayo pale Arsenal. Kinachomfanya ajitoe na kufanya vizuri ni kujaribu kudumu kwenye nafasi ambayo Klopp amekuwa akimpa acheze, nayo ni kama kiungo wa katikati huku akijua kuwa kuna watu wengine wanampa ushindani mkubwa hapo.
Ox amekuwa na uhakika wa kuanza mara kadhaa mbele ya watu kama kina Emre Can, Georginio Wijanaldum na hata Adam Lallana kutokana kasi kubwa aliyonayo. Silaha yake kubwa alionayo Ox ni kasi yake. Na hii ndio inampa faida kubwa ya kuanza mbele ya wengine kutokana na uhitaji wa falsafa za Klopp ya Gengenpressing ambayo inahitaji wachezaji wenye kasi na wanaoweza kukimbia muda wote wa dakika 90 pasi na kuchoka na hapa ndipo Ox anapofaidika.
Kucheza pembeni mara nyingi kwenye kile kiungo cha kati kimetokana na uhitaji wa yeye kupunguza presha kwa mabeki wa pembeni dhidi ya viungo wa kati wenye kasi. Ox kwa sasa anakua na anaaza kuelewa kuwa kasi yake ndio inampa kipaumbele tena kwenye eneo la kiungo. Kasi hii ndio ilimfanya apewe mbavu za pembeni pale Arsenal akimbize Wingback lakini mfumo wa Klopp unahitaji watu wenye kasi na ndio umekuwa ukimpa kipaumbele pale katikati dhidi ya wengine.
Alichotuaminisha Ox pale Arsenal ni kuwa anachoweza kukifanya ni kukimbia na kutia krosi lakini kumbe ana uwezo pia wa kufunga na kutoa pasi za magoli. Ile ile kasi yake ambayo aliitumia kukimbia peke yake ndio ambayo sasa anaitumia kuingia kwenye nafasi na kutafuta nafasi za kufunga. Kimfumo Liverpool haitumii mawinga wa asili na hii huwa inatoa nafasi kwa wachezaji kuweza kuingia kwenye nafasi yoyote pale mbele.
Mabadiliko yake kiuchezaji yameonekana kuwa makubwa, kitendo cha kucheza pale kati kimetoa nafasi kwake kufika kwa urahisi kwenye lango la wapinzani na kupata nafasi pia ya kupiga mashuti na haishangazi ana magoli kadhaa kutoka nje ya eneo la 18. Hali ya kujiamini imeonekana kuwa kubwa na anaonekana kutokuwa na papara na kufanya maamuzi kwa utulivu na hata krosi zake nyingi zimeonesha kuwa tishio na amekuwa akifanya maamuzi mazuri karibu na lango la adui iwe kwenye kupiga mashuti yenye kulenga lango au kutoa pasi kwenye nafasi.
Haya ndio mabadiliko yenye kuleta matumaini kwake. Alionekana kama usajili wa ajabu hivi lakini Ox anaitumia vizuri nguvu yake kubwa ambayo ni kasi yake kuanza kuwalipa Liverpool kila pauni walioitumia kumsajili majira ya kiangazi. Ox wa sasa ni tishio uwanjani lakini Klopp ni mwalimu ambaye amekuwa na kawaida ya kuwabadilisha sana wachezaji. Alifanya hivyo kwa wengi pale Dortmund na Ox anaonesha mabadiliko. Yajayo yanafurahisha Kops. Ox anakuja vizuri . cc Haatim Abdul
No comments