OMOG; NIMEANDAA MKAKATI MAALUMU ZIDI YA MBEYA CITY NA TANZANIA PRISONS
Kocha wa Simba Joseph Omog, ameandaa mpango mkakati maalumu ambao utakiwezesha kikosi chake kuibuka na pointi sita kwenye mechi mbili wanazokwenda kucheza nyanda za juu Kusini.
Omog amesema amepania kuhakikisha timu yake inavunja rekodi ya Yanga kwa kushinda mechi hizo mbili ingawa amekiri kuwa siyo jambo dogo.
“Msimu uliopita tulijitahidi kufanya hivyo lakini ilishindikana msimu huu tunaanza tena kucheza ugenini mechi zote mbili kwa ubora wa kikosi tulichokuwa nacho naamini tunaweza kuvunja rekodi ya Yanga,” amesema Omog.
Kocha huyo raia wa Cameroon, amesema moja ya kitu ambacho kinampa uhakika wa kushinda mchezo huo ni ari waliyokuwa nao wachezaji wake pamoja na maandalizi ambayo wanaendelea kuyafanya hadi sasa.
Omog amesema anaziheshimu sana Mbeya City na Tanzania Prisons, lakini msimu huu ataomba wawasamehe kwani wamejipanga kuhakikisha wanarudisha heshima na hadhi ya Simba.
Simba inatarajiwa kuondoka Dar es Salaam, siku yoyote kuanzia kesho kuelekea Mbeya ambapo Jumapili, itashuka kwenye dimba la Sokoine kucheza na Mbeya City na baada ya mchezo huo itaendelea kubaki huko mpka Jumamosi ijayo itakapo cheza na Tanzania Prisons kwenye uwanja huo huo.
No comments