Breaking News

SIMBA YAPIGWA FAINI NA TFF

RAIS WA TFF WALLACE KARIA.  

KLABU ya Simba imelimwa faini ya Sh. 500,000 kutokana na kitendo chao cha kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanjani kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC. 

Mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa, ililazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji wao hao. 

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kitendo hicho cha Simba ni ukiukwaji wa Kanuni ya 14 ya Ligi Kuu, na adhabu dhidi yao ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu. 

Pia aliyekuwa kamishna wa mechi hiyo, Maliki Tibabimale, amepewa onyo kali kwa kutoripoti kitendo hicho cha Simba. 

Katika mchezo huo ulikokuwa na upinzani mkubwa, Simba walitangulia kufunga mara mbili, lakini Mbao FC walipambana na kusawazisha mabao hayo hivyo kila timu kuondoka na pointi moja. 

Kikosi cha Simba kwa sasa kipo katika maandalizi ya kuvaana na Mtibwa Sugar Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaa, 

Rungu la TFF pia limezikumba klabu za Singida United iliyopigwa faini ya Sh. 500,000 kutokana na mashabiki wa timu hiyo kuingia uwanjani kushangilia baada ya mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyofanyika Septemba 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. 

Pia Stand United imepigwa faini ya Sh. milioni moja kutokana na mashabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Mbeya City na Simba, zote zilichezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. 

Katika mechi namba 31 iliyofanyika Septemba 24 , mashabiki hao waliwafanyia vurugu wachezaji wa Mbeya City wakati wakielekea vyumbani baada ya mchezo kumalizika, kabla ya Polisi kuingilia kati na kuwatawanya.


No comments