HAJI MANARA; HATUHUSIKI NA MABADILIKO YA RATIBA SIMBA
SIKU moja baada ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), kutoa ratiba mpya ya Ligi Kuu iliyofanyiwa marekebisho, uongozi wa klabu ya Simba umesema haijashinikiza mabadiliko hayo kama inavyodaiwa na baadhi ya wadau wa soka.
Baada ya TFF kusogeza mbele michezo iliyokuwa ichezwe leo ikiwamo mechi yao dhidi ya Azam na kusogezwa hadi Jumamosi, baadhi ya mashabiki walilalamika kuwa mabadiliko hayo yamelenga kuisaidia Simba ambao wanasubiri kurejea kwa nyota wao wa wawili, Juuko Murshid na Emmanuel Okwi waliopo kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda ambacho leo kinacheza na Misri.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara, alisema Simba haihusiki na mabadiliko hayo ya ratiba ya ligi.
“Huku ni kushinikiza mambo, naomba niweke wazi klabu ya Simba haihusiki na mabadiliko haya, watu wanaosema mabadiliko haya ni kwa ajili ya kuisaidia Simba ni wazushi na si wanamichezo,” alisema Manara.
Alisema wanaamini mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na ratiba ya awali kuingiliana na michezo ya kimataifa ya Kalenda ya Shirikisho la Soka duniani (Fifa).
“Taratibu zinataka kunapokuwapo na mashindano ya Fifa, hakupaswi kuwa na michezo mingine ya ligi, tunaona hili hata kwa wenzetu Ulaya sasa sisi Simba tunaingizwaji hapo,” aliongeza kusema Manara.
Mabadiliko ya Ratiba yanaonyesha Simba itaifuata Azam kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex Jumamosi ijayo huku pia mchezo wao dhidi ya watani zao, Yanga ukisogezwa mbele kwa wiki mbili kutoka Oktoba 14 mpaka Oktoba 28, mwaka huu.
No comments