Breaking News

ASLAY; SINA NILICHO KIKOSA BAADA YA KUVUNJIKA KWA KUNDI



Mwanamuziki wa Bongo Fleva anayeongoza kwa kupachikwa majina mbalimbali na kufananishwa na wasanii wakubwa kimataifa akiwemo Chris Brown, Aslay Isihaka ‘Fundi’, amesema kuwa baada ya kundi lao la Yamoto Band kuvunjika, yeye anaendelea vizuri na kazi zake wala hamna anachokikosa kwa sababu wakati anaanza hakuwa na kundi.

Aslay ambaye kwa sasa anatamba na ngoma zisizohesabika kama vile, Likizo, Baby, Pusha, Nyakunyaku, Mhudumu na nyingine nyingi, alisema kuwa:
“Nilianza muziki nikiwa peke yangu na nilikuwa mdogo kiumri, enzi zile za ‘Naenda Kusema kwa Mama’, ila niliweza kufanya vizuri, kwa hiyo kuingia kwenye kundi na kutoka sioni kama nitashindwa kuendeleza muziki wangu.

“Kwa sababu naona ni kama zamani tu, ndiyo maana nafanya vizuri, naachia ngoma kila kukicha, na ngoma zangu kali na zinapendwa, mashabiki hawawezi kuzichoka kwa sababu mimi ni mwanamuziki mzuri, najua nini ninachokifanya, na sitegemei kushuka kimuziki.”
Aslay ni mmoja kati ya wanamuziki waliokuwa wakiunda kundi la Yamoto Band, kundi ambalo lilifanya vizuri sana ndani na nje ya nchi, kupitia nyimbo zao kali kama Nitakupwelepeta, Cheza kwa Madoido, Niseme Nisiseme na Su waliyomshirikisha mwanadada Ruby.


No comments