Breaking News

Nusu ya waliofariki na mafuriko Sierra Leone

Maafisa wa afya nchini Sierra Leone, wamesema karibu nusu ya watu 400, ambao wametambulika kufariki dunia kutokana na maporomoko ya udongo na mafuriko nje kidogo ya mji mkuu wa nchi hiyo Freetown, wamezikwa tayari

Serikali ya nchi hiyo imesema mazishi ya halaiki ambayo awali yalipangwa kufanyika jana Jumatano, yanaweza kuahirishwa ili kutoa fursa kwa ndugu kuwatambua wapendwa wao.

Mkuu wa uchunguzi kuhusu magonjwa jijini Freetown, ameliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kwamba baadhi ya mazishi tayari yameshafanyika.

Bado watu takribani 600, hawajulikani walipo kutokana na dhahama hiyo iliyoacha majonzi makubwa nchini humo.

Rais wa nchi hiyo, Ernest Bai Koroma, ametangaza siku saba za maombolezo huku akiomba msaada wa haraka juu ya tukio hilo.

Mazishi ambayo tayari yamefanyika, yamehusisha miili ambayo imetambulika au ile ambayo imeharibika vibaya.

No comments