Umesikia alichokisema Tambwe kuhusu Himid Mao?
Mshambuliaji wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe.
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe, amesikia taarifa za kiungo mkabaji wa Azam FC, Himid Mao kutua katika timu hiyo akafurahi na kutamka: “Tukimpata huyo tutakuwa tumemaliza kazi na watatutambua.” Kiungo huyo, ni miongoni mwa wachezaji waliopo kwenye orodha ya nyota wanaowindwa na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara pamoja na Mrundi, Yusuph Ndikumana na Mcongo, Kasaka Tshishimbi.
Yanga ipo kwenye mazungumzo na viungo hao wote wakabaji kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Mzambia, Justine Zulu ‘Mkata Umeme’ aliyeonyesha kiwango kidogo. Akizungumza na Championi Jumatano, Tambwe alisema kiungo huyo ndiye anayehitajika kutokana na kukidhi vigezo vinavyohitajika kucheza nafasi hiyo.
Tambwe alisema, uongozi wake huo kama ukikamilisha usajili wa kiungo huyo, basi uachane na viungo hao wakabaji wanaowahitaji kwa ajili ya kuwasajili kutoka nje ya nchi. Aliongeza kuwa, Himid ni kati ya viungo bora anaowakubali kutokana na uwezo wake wa kukaba na kuchezesha timu wakati timu ikiwa na mpira.
“Yanga tulikuwa na tatizo la muda mrefu kwenye safu ya kiungo mkabaji, ingawa waliokuwepo walikuwa wapo vizuri. “Nimesikia taarifa za uongozi kuwepo kwenye mazungumzo ya mwisho na Himid, binafsi nawaambia wamalizane naye haraka kama mkataba wake umemalizika Azam.
“Ninaamini kama tukimpata huyu, basi kazi imemalizika na uongozi usitishe mpango wa kumsajili kiungo mkabaji kutoka nje ya nchi,” alisema Tambwe.
No comments