Breaking News

Umesikia alichokisema Ajibu kuhusu Yanga

SIKU chache baada ya kukamilisha usajili wa kujiunga na mabingwa wa soka Tanzania, Yanga, mshambuliaji Ibrahim Ajibu, amesema kuwa moja ya sababu ya kujiunga na timu hiyo ni kufuata makombe. 

Ajibu, aliiambia Nipashe kuwa mashabiki wa timu hiyo wategemee mambo makubwa kutoka kwake kwa kuwa amedhamiria kuhakikisha yeye pamoja na wachezaji wenzake wanaifikisha mbali timu hiyo. 

"Nashukuru kwa sasa mimi ni mchezaji wa timu yenye mafanikio zaidi Tanzania.. binafsi nataka kuweka rekodi yangu nikiwa hapa kwa sababu tayari nimeikuta Yanga ikiwa na rekodi ya kutwaa makombe mengi zaidi hapa nchini," alisema Ajibu. 

Alisema amefurahi namna alivyopokelewa na mashabiki wa timu hiyo na anajiona ana deni la kuwalipa pindi atakapoanza kuichezea timu hiyo kwenye Ligi Kuu na michuano ya Kimataifa. 

"Mapokezi ya mashabiki na namna wanavyonizungumzia kwangu nataka kuwalipa yote hayo kwa kufanya vizuri na kutwaa makombe mengi zaidi," alisema mshambuliaji huyo. 

Katika hatua nyingine, Ajibu hakuacha kuwashukuru mashabiki wa timu yake ya zamani ya Simba kwa ushirikiano na sapoti waliyompa kwa muda wote akiwa ndani ya kikosi cha timu hiyo. 

"Nimeishi vizuri Simba..., ingawa kwa sasa mimi ni mchezaji wa Yanga lakini mashabiki wa Simba na viongozi wote nawashukuru kwa sapoti yao," aliongezea kusema Ajibu. 

Msimu uliopita Ajibu alikuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo na waliochangia kuifanya Simba kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi pamoja na kutwaa ubingwa wa kombe la FA. 

Nyota huyo Jumatatu ataanza rasmi mazoezi na timu ambayo imepanga kufanya mazoezi kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola akiwa pamoja na wachezaji wengine waliosajiliwa hivi karibuni kuitumikia klabu hiyo.

No comments