SIMON MSUVA: NIKICHEMKA MOROCCO NARUDI YANGA
HUSSEIN OMAR NA ZAITUNI KIBWANA
KIUNGO Simon Msuva, ambaye anahesabu siku chache tu kujiunga na klabu yake mpya ya Difaa El Jajida, inayoshiriki Ligi Kuu nchini Morocco, amesema atarejea kwenye klabu yake ya Yanga kama malengo yake hayatatimia.
Msuva, aliyeanza kuitumikia Yanga tangu mwaka 2013, akitokea klabu ya Moro United, anatarajia kuanza maisha mapya ya soka la kulipwa katika timu hiyo, ambayo kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, inayojumuisha timu 16.
Akizungumzia safari yake ya nchini Morocco, Msuva alisema mipango yote imekamilika na sasa anasubiri viza ambayo itatoka ndani ya wiki hii.
“Nasubiri viza itoke ili nitumiwe tiketi ya kwenda nchini Morocco, tayari nimeshazungumza na Yanga na wamekubali, hivyo kila kitu kinakwenda sawa.
“Kila jambo ni kumuomba Mungu, naamini malengo niliyojiwekea yatatimia, lakini yasipotimia basi nitarejea Yanga, ambako nimecheza kwa miaka mitano,” alisema Msuva.
Kuondoka kwa kiungo huyo, ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Yanga, kumeitajirisha klabu yake kwa dau nono la Dola 80,000 za Marekani (Sh milioni 177), ambalo watalipwa katika makubaliano ya awali na klabu ya Difaa El Jajida.
Msuva anatarajia kulipwa mshahara wa Dola 4,000 za Marekani, sawa na Sh milioni 8.8 kwa kila mwezi na katika kikosi cha Difaa El Jajida ataungana na Mtanzania mwenzake, Ramadhan Singano ‘Messi’, ambaye naye amesajiliwa.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, amemtakia Msuva mafanikio mema katika maisha yake mapya na kumtaka apambane kufa na kupona kuhakikisha anapiga hatua zaidi.
“Namtakia kila la heri akapambane kwa kila kitu, ili aweze kutoka na baadaye tumsikie akiwa kwenye klabu kubwa barani Ulaya,” alisema.
No comments