Messi aongeza mkataba Barcelona hadi 2021
MSHAMBULIAJI wa Barcelona, Lionel Messi amekubali kuongeza mkataba na klabu hiyo hadi mwaka 2021.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30, aliyejiunga na Barca akiwa ana umri wa miaka 13, atasaini mkataba huo atakaporejea mazoezini kutoka mapumzikoni.
"Klabu ina furaha sana kwa Messi kukubali kusaini mkataba mpya, mchezaji bora kihistoria,"imesema kalbu hiyo ya La Liga.
Mshambuliaji huyo wa Argentina ameifungia klabu hiyo mabao ya rekodi 507 katika mechi 583 tangu aanze kuichezea mwaka 2004.
Messi, ambaye kwa sasa yupo fungate baada ya kufunga ndoa na mpenzi wake wa tangu utotoni, Antonela Roccuzzo, pia anashikilia rekodi ya mabao La Liga akiwa amefunga mabao 349.
Vyombo vya Habari Hispania vimesema kwamba mkataba mpya unahusisha kipengele cha kuuzwa kwa Pauni Milioni 263 na kimewekwa baada ya Messi kuripotiwa kugomea ofa ya awali mwezi Mei.
Mkataba wa sasa wa Messi unamalizika mwaka 2018 na mchezaji huyo awali alihusishwa na kuhamia Manchester City, lakini mkataba wake mpya utamuweka na mabingwa mara 24 wa La Liga hadi atakapofikisha umri wa miaka 34.
Tangu apandishwe kikosi cha kwanza chini ya kocha wa wakati huo Barca, Frank Rijkaard, Messi ameshinda mataji nane ya La Liga, manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na matano ya Copa del Rey.
No comments