Breaking News

KAMBI YA SIMBA YANOGA

wachezaji wa klabu ya Simba waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars wamewasili leo mjini Johannesburg, Afrika Kusini kujiunga na kambi ya timu yao kwa maandalizi ya msimu mpya.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online kwamba kipa Aishi Manula hajakwenda kwa sababu hajamaliza mkataba wake na klabu yake, Azam FC lakini kipa mwingine mpya, Said Mohammed aliyesajiliwa kutoka Azam FC amekwenda.

Kutoka kulia John Bocco, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin na Salim Mbonde baada ya kuwasili Afrika Kusini leo na kuanza mazoezi na wenzao

Manara amewataja wachezaji wengine waliokwenda Afrika Kusini leo ni mabeki Erasto Nyoni, Shomari Kapombe waliosajiliwa kutoka Azam FC, Salim Mbonde aliyesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar, viungo, Muzamil Yassin, Shiza Kichuya, Said Ndemla na mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’ aliyesajiliwa kutoka Azam FC pia.  
Nyota hao walikuwa kwenye kikosi cha Stars kilichotolewa mapema kwenye michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayoshirikisha wachezaji wanaocheza nchini mwao pekee, baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 na wenyeji Rwanda Uwanja wa Kigali, uliopo Nyamirambo mjini Kigali Jumamosi.
Kwa matokeo hayo, Taifa Stars imetolewa kwa bao la ugenini, kufuatia kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Jumamosi ya wiki iliyotangulia.
Na baada ya matokeo hayo, wachezaji wa kikosi cha kocha Salum Mayanga, ambacho wiki mbili zilizopita kilishinda Medali ya Shaba kwenye michuano ya COSAFA Castle mjini Rusternburg, Afrika Kusini wanarejea kwenye klabu zao kwa maandalizi msimu mpya. 
Wanaungana na wenzao waliotangulia ambao ni kipa Emmanuel Mseja, mabeki Jamal Mwambeleko waliosajiliwa kutoka Mbao FC, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Yussuf Mlipili aliyesajiliwa kutoka Toto Africans, Ally Shomari aliyesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar, Method Mwanjali, viungo Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, James Kotei, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim na washambuliaji Laudit Mavugo na Juma Luizio
Simba itarejea Dar es Salaam siku chache kabla ya Tamasha kubwa la kila Mwaka la Simba Day, lililopangwa kufanyika kama kawaida Agosti 8, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Siku hiyo Simba itatambulisha kikosi chake kamili cha msimu kabla ya kucheza mechi ya kirafiki na timu moja kutoka nje, baada ya kutwa iliyopambwa na burudani mbalimbali, ikiwemo zoezi la kuwauzia jezi mpya wapenzi na wanachama wa timu hiyo.

No comments