Omog ataka ripoti yake kufanyiwa kazi
Bosi wa benchi la ufundi la Simba, Joseph Omog raia wa Cameroon, amesema kuwa, anataka kuona uongozi unafanya usajili kutokana na kile alichokibainisha kwenye ripoti yake aliyoiwasilisha hivi karibuni na si kwa matakwa yao binafsi.
Simba ambayo juzi Alhamisi ilitangaza rasmi kuingia mkataba wa miaka miwili na Jamal Mwambeleko aliyetoka Mbao FC, huku ikimpa mkataba wa miaka mitatu sambamba na Yusuph Mlipili aliyekuwa Toto Africans, imepanga kufanya usajili wao kwa umakini kuepuka kuwa na wachezaji wengi wasiokuwa na msaada.
Omog amesema anataka kuona ripoti yake inafanyiwa kazi kwa kusajiliwa wachezaji watakaotumika na si kukaa benchi ili kutimiza malengo ya klabu ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya kuukosa kidogo msimu uliomalizika hivi karibuni.
“Mwongozo wa nini kifanyike kwenye kikosi changu kwa ajili ya msimu ujao nimeweka kwenye ripoti, hivyo ni jukumu la uongozi kuangalia na kufanyia kazi.
“Kama ripoti ikifanyiwa kazi ipasavyo, naamini msimu ujao tutafanya vizuri zaidi kuliko msimu uliokwisha, hatutaki kuwa na wachezaji wengi halafu hawatumiki.
"Wote watakaosajiliwa basi ni lazima waonyeshe mchango wao kwenye timu na hapo ndipo tutafikia malengo kwa pamoja,” alisema Omog.
No comments