Watu 22 Wauawa Kwa Bomu Manchester, Uingereza
Watu 22 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa vibaya kwenye shambulio baya la bomu lililotokea kwenye ukumbi lilipokuwa likifanyika tamasha la muziki la mwanamuziki Ariana Grande, jijini Manchester, Uingereza.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May ametaja tukio hilo kama kitendo cha ugaidi. Ikiwa itathibitishwa kuwa ni shambulio la kigaidi, litakua ni shambulio baya zaidi kuwahi kuikumba Uingereza tangu Julai, 2005 ambapo watu 50 walikufa kwenye mfululizo wa milipuko jijini London.
Watu walioshuhudia mlipuko huo wa Manchester, wamesema mwanamuziki wa Marekani, Ariana Grande alikuwa amemaliza kutumbuiza mbele ya mashabiki wake, wakati mlipuko mkubwa uliposikika na kutikisa ukumbi mzima.
Mashahidi wamesema waliona misumari iliyotapakaa sakafuni na harufu ya vilipuzi.
Eneo kulikotokea mulipuko huo limezingirwa na polisi waliojihami wanaendelea kushika doria.
No comments