Kessy amemvika Niyonzima ufalme wa VPL
Beki wa Yanga, Hassan Kessy amemtaja mchezaji mwenzake wa timu hiyo, Haruna Niyonzima kuwa ndiye anayestahili kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Kessy amemtaja Niyonzima ikiwa ni siku chache tu baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuyaweka hadharani majina ya wachezaji watano watakaowania tuzo hiyo.
Wachezaji hao ni Aishi Manula kutoka Azam FC, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Shiza Kichuya (wote kutoka Simba) na Simon Msuva na Haruna Niyonzima wa Yanga.
Shaffihdauda.co.tz ilizungumza na Hassan Kessy kabla hajaondoka kuelekea Mwanza kwenye mchezo wao dhidi ya Mbao na akasema Niyonzima ni moja ya viungo hapa Tanzania ambao anawaheshimu na anafurahi kucheza nae timu moja.
“Ni mchezaji mwenye uwezo wa juu sana, muda wowote anaweza kufanya kitu ambacho hukutarajia na kuisaidia timu yake, yaani namfananisha na Iniesta wa Barcelona,” amesema Kessy.
Mchezaji huyo wa zamani wa Simba itakuwa mara yake ya kwanza kushinda taji la VPL ikiwa timu yake itapata matokeo ya ushindi au sare dhidi ya Mbao kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
No comments